Tanzania Red Cross Society inayojulikana na wengi kama Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania ni moja ya mashirika ya Kibinadamu yenye wahudumu wa kujitolea yaani “Volunteers” ambalo lilianzishwa mahsusi ili kulinda masilahi ya afya ya binadamu, kuhakikisha heshima kwa hulka ya mwanadamu na kupunguza mateso ya kibinadamu bila ubaguzi wowote kwa misingi ya Utaifa, Rangi, Jinsia, Imani za kidini, Daraja la kijamii au maoni ya kisiasa.
Red Cross Society inaongozwa kwa misingi ya sheria na kanuni, moja ya kanuni zao za msingi kabisa ni ‘Kujitolea’, kwa kutumia kanuni Wanachama/Wahudumu wa Red Cross (Volunteers) huwa wapo tayari kujitolea kwa kutoa huduma au misaada ya kibinadamu mahali popote, wakati wowote na kwa watu wote hususani yanapotokea majanga kama vile Ajali, Moto, Njaa, Mafuriko, Vita n.k.
Kujitolea ndiko kulikowafanya Red Cross kuweka kambi Wilayani Kibiti kuanzia tarehe 10 Aprili, 2024 mpaka leo ili kutoa msaada kwa waathirika wa mafuriko yaliyoikumba Wilaya hii, na waliokuja kutoa msaada ni Volunteers wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Baada ya kufika Kibiti Bi. Chandama Bakari ambaye ni Mjumbe wa jinsia kamati tendaji ya Mkoa na pia ni team leader wa Volunteer wa Dar es Salaam waliokuja kukabiliana na mafuriko Kibiti na Rufiji aligundua kutokuwepo kwa wanachama wa Red Cross Kibiti jambo lililosababisha uchelewaji wa msaada kwa waaathirika.
Bi. Chandama alipeleka ujumbe kwa viongozi wake na Jana tarehe 05 JUNI, 2024 tumeona matunda ya ujumbe huo kwa kufunguliwa kwa tawi la Red Cross Wilayani Kibiti.
Akifungua tawi hilo Mkurugenzi wa matawi ya Red Cross society Tanzania Bw. Reginald Mhango, amewashukuru viongozi wa Wilaya ya Kibiti kwa kuwapokea vyema na kutoa ushirikiano tangu walipofika mpaka leo lakini zaidi kwa kuridhia uanzishwaji wa tawi hili la Red Cross Society Kibiti.
Bw. Mhango pia amewashukuru Volunteers waliojitokeza kwaajili ya Kibiti.
“Niwapongeze sana kwa kujitokeza ili kusaidia watu kwa kazi hii isiyo na mshahara, nawaomba tujitolee kwa moyo wa dhati kabisa. Sitaki kuwaahidi makubwa tufanye kazi kwa bidi siku yeyote neema inaweza kushuka naamini hamtojutia kuwepo Red Cross” Alisema Bw. Mhango
Akisoma Risala kwa mgeni rasmi mmoja wa Volunteers wa kibiti Bi. Marygoreth Francis Leula amesema kipekee wanamshukuru Madam Grace Mawalla kiongozi wa Red Cross Mkoa wa Dar es Salaam na ambaye anakaimu Mkoa wa Pwani kwa sasa na Mratibu wa uanzishwaji wa matawi mapya akisaidiwa na kikosi kazi cha watu zaidi ya 30 kwa kuwakimbilia wakati wa mafuriko na kusimamia uanzishwaji wa tawi hili.
“Tunaahidi kwamba tupo tayari kuitumikia jamii ya Kibiti na Rufiji na Tanzania kwa ujumla wakati wowote/mahali popote/kwa watu wote bila kubagua na kwa misingi na kanuni za chama cha Red Cross ulimwenguni” Alisema Bi. Marygoreth
Akifunga hafla hiyo kwa niaba ya mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Kibiti, Bw. Gideon Matwi ambaye ni Mratibu wa maafa Wilaya ya Kibiti amewashukuru viongozi wa Red Cross society Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuanzisha tawi Kibiti huku akiahidi kuwa Wilaya itatoa ushirikiano kwa shirika hilo kadri itakavyohitaji.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.