Tarehe 9/01/2023 Baadhi ya Walimu wa shule za Sekondari za Wilaya ya Kibiti wamekutana katika ukumbi wa Halmashauri kujadili namna ya kupeana uzoefu wa utungaji wa mitihani na ujibuji wa maswali ikiwa ni kikao kazi chenye mkakati wa kuongeza uelewa na ufaulu wa mitihani kwa Wanafunzi wa Sekondari.
Akiongoza mkutano huo Afisa Elimu Anna Shitindi amesema lengo la kukutana ni kubadilishana uzoefu ili kuwajengea Walimu wengine uelewa waweze kuendana na mfumo mpya wa “Compitence based approach” baada ya kuhama katika mfumo wa zamani (content based) kutokana na wengi wao kutopata mafunzo hayo.
“Tushikamane, tushirikiane kuhusu kujikwamua ili tuweze kufikia malengo”alisema Shitindi.
Hata hivyo Shitindi amewaagiza Walimu wote kuhakikisha wanakutana na wanafunzi kuwapa mwelekeo wa namna ya kujibu maswali wakati wa mitihani kwa kufuata mpangilio mzuri ambao utasaidia wanafunzi kufanya vizuri na kupata ufaulu.
Katika mkutano huo ulioendeshwa Kwa njia ya majadiliano Walimu wamesema wanakutana na changamoto nyingi katika mazingira ya kazi kubwa zaidi ni kutoka kwenye Jamii inayowazunguka .
Vilevile wamesema changamoto nyingine zinazofanya wanafunzi wasifaulu ni uelewa mdogo wa lugha ya kufundishia, walimu kutomaliza silabasi,wanafunzi kutofanya mzoezi ya kutosha darasani,Walimu kutokuwa na mbinu mpya za ufundishaji na zaidi ni upungufu wa vitabu vya kufundishia mashuleni. Na upungufu wa walimu ukilinganisha na idadi kubwa ya wanafunzi.
Aidha baada ya majadiliano Afisa Elimu Shitindi na Walimu wote katika kikao hicho ili kufika malengo kwa pamoja wameazimia kuwa tayari kubadilishana uzoefu wa namna ya kutunga maswali kwa mfumo wa Compitence based approach, kutia mkazo katika somo la lugha ya kingereza kwa Walimu na wanafunzi katika kufundisha na kujifunza na kuzingatia kufundisha kulingana na Mazingira yanayowazunguka (realia).
Vile vile wameazimia kuzingatia matumizi ya vitabu vya kiada kutoka (TET), wanafunzi kusisitizwa kuzingatia maelekezo ya mtihani, Walimu kuhakikisha wanamaliza mada zilizopangwa wa muda muafaka, wanafunzi kujibu maswali ya mtihani kwa kuzingatia mpangilio mzuri wa kazi na majibu yanayosomeka bila kuacha swali na kuunda vikundi vya wanafunzi wenye uelewa wa juu na wenye uelewa wa chini kwa lengo la kuwaunganisha ili waweze kusaidiana wao kwa wao n.k.
Katika Mkutano huo mwisho Walimu wamegawana majukumu kwa kugawiwa katika makundi tayari kwa kuwezesha Walimu wengine kuanza kubadilishana uzoefu .
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.