Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mwl. Anna Shitindi amewataka Maaafisa Elimu Kata na Wakuu wa Shule kuzitumia vema timu za udhibiti ubora wa shule wa ndani ya shule kwani zikijua majukumu yao na kutumika ipasavyo zitakuwa ni msaada mkubwa sana katika ufuatiliaji wa kitaaluma shuleni.
Mwl. Shitindi amesema hayo katika Kikao cha kutathmini mikakati ya kuinua taaluma Wilayani Kibiti kilichofanyika leo Julai 11, 2024 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti. Kikao hicho kimehusisha Idara ya Elimu Sekondari (W), Wakuu wa Shule zote za Sekondari na Maafisa Elimu Kata wote Wilayani Kibiti.
Katika kikao hicho wakuu wa shule wamewasilisha taarifa ya mafanikio, mikakati ya kuinua ufaulu pamoja na changamoto wanazokutana nazo kwenye suala zima la kuinua taaluma katika shule zao. Walimu hao wamewataka wazazi kutoa kushirikiana kikamilifu na walimu ili kutimiza ndoto za wanafunzi kuanzia suala la kuchangia chakula, kudhibiti utoro na kusimamia sheria ambazo zitapunguza idadi ya mimba shuleni.
Aidha walimu hao wameomba kupelekewa umeme kwenye shule ambazo mpaka sasa hazina umeme ili kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na uwezo wa kujisomea nyakati zote pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa shule kama uzalishaji wa mitihani.
Akifunga kikao hicho Mwl. Shitindi amewataka walimu wote kuhakikisha ufaulu unaishia daraja la 2 na si vinginevyo, lakini pia kila shule kuhakikisha inakuwa na viwanja na vifaa vya michezo yote kwakuwa michezo ni sehemu ya Elimu.
“Sitarajii kuona daraja la tatu, Wafikishieni salamu walimu wote kwamba ni ufaulu wa daraja la kwanza, daraja la pili la kutafuta kwa tochi na daraja la tatu ni marufuku” Alisema Mwl. Shitindi
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.