31/3/2023.
Katika kuadhimisha siku ya afya na lishe ya Kijiji, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imeendelea na zoezi la kutoa elimu kwenye Jamii juu ya umuhimu wa lishe na namna ya kuandaa lishe yenye mlo kamili.
Akitoa mwongozo wa ulaji Afisa Lishe wa Wilaya Ndg, Samson Minja amesema kila mtu awe mkubwa au mdogo anapaswa kula vyakula vya aina mbalimbali kutoka katika makundi tofauti ya vyakula kila siku ili aweze kuwa na afya njema na mwenye nguvu kwani, chakula cha mchanganyiko husaidia mwili kupata virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini.
Vilevile Minja amesema katika kuhakikisha ukuaji mzuri wa mtoto, baada ya kuzaliwa anatakiwa kunyonya maziwa ya mama yake kwa miezi 6 bila kumpa chakula cha nyongeza kwasababu maziwa ya mama ni kinywaji na chakula pekee chenye virurubisho vyote muhimu kwa ajili ya ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili.
Hata hivyo Minja amefafanua kwamba,baada ya mtoto aliyezaliwa kutimiza miezi 6,ni wakati muafaka wa kuanza kupewa chakula mchanganyiko ikiwa ni pamoja na jamii ya kunde,matunda,mbogamboga na matunda huku akiendelea kunyonya maziwa ya mama mpaka atakapotimiza miaka 2-3 kwa afya bora yenye ukuaji mzuri wa mtoto kimwili na akili pia.
Aidha Afisa lishe huyo amewaelekeza wazazi na wajawazito namna ya kuandaa lishe iliyosheheni mlo kamili kwani wengi wao huandaa lishe yenye vyakula vya kundi moja pekee bilakujua kama wamefanya hivyo.
“Kila unapoandaa lishe bora hakikisha una Mahindi ya njano ambayo hayajakobolewa,soya iliyokobolewa robo,mbegu za za maboga robo na ufuta robo” alisema Minja huku akisisitiza kwamba,ukitengeneza lishe yenye aina hizo 4 za vyakula, utakuwa umeandaa lishe iliyojitosheleza.
Mwisho Minja amewataka wazazi/walezi kuhakikisha wanatunza vyakula katika mazingira makavu yenye hali ya usafi na usalama.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.