15.5.2024
Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Thabit Mlindo akiwa ameambatana na Kaimu Mwenyekiti na Katibu wa Bakwata (w) wamemkabidhi misaada ya kibinadamu Mkuu wa Wilaya ya Kibiti kwa ajili ya kuwapa pole waathirika wa mafuriko wilayani humo, sambamba na kutoa pole kwa nchi nzima kwa wananchi waliopatwa na Mafuriko.
Misaada iliyotolewa ni nguo mchanganyiko mafurishi 8, ndoo 1 tupu ya lita 20, ndoo ndogo 7 za lita 10, sufuria PC 5, bakuli PC 3 na vikombe PC 3.
Akikabidhi misaada hiyo Shekhe Thabit ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Amani (W) amesema msaada huo ni sehemu ya harambee ya michango kutoka Ofisi ya Bakwata na waumini (wananchi) walioguswa kuwapa pole ndugu zao katika kipindi hiki cha mafuriko.
Katika kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Shekhe Thabit ametoa wito kwa wanajamii wengine kuendelea kuguswa na kuwafariji waliofikwa na changamoto hiyo kwani kusaidiana ni sehemu ya Ibada hivyo binadamu wanapaswa kuhurumiana.
"Tuchangie na kuwahudumia wenzetu kwa kuwakumbuka na kuwahurumia kwa sababu maandiko yanasema anayehurumia naye uhurumuwa na Mwenyezi Mungu" Alisema.
Akipokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo akiwa ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama (W) amewashukuru Bakwata kwa msaada walioitoa na kuonyesha moyo wa huruma kwa waathirika wa Mafuriko hayo yaliyotokana na kuongezeka kwa maji katika mto Rufiji kutokana na mvua kubwa zilizonyesha nchini.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.