Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Meja Edward Gowele amewataka wawekezaji,wafanyabiashara na sekta binafsi wa Wilaya ya Kibiti kutumia fursa ya bonde la mto Rufiji kuzalisha mazao kwa wingi kwani hekari 400 zilizopo zinafaa kwa kilimo.
“Tumieni fursa ya bonde la mto Rufiji kuzalisha mazao kwani , hekari takribani 400 zilizopo zinafaa kwa kilimo”Alisema Gowele .
Amesema hayo alipokuwa kwenye kikao cha Baraza la Biashara la wilaya lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo ambapo wadau wote kwa pamoja wameridhia ajenda zote zilizokuwa zikijadiliwa.
Meja Gowele ambaye ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema licha ya changamoto zilizopo, shirikianeni kwa pamoja huku akisisitiza wajumbe kutumia fursa ya Baraza hilo kugusa maeneo muhimu kwa njia ya majadiliano kutatua changamoto huku akisisitiza Taasisi za TARURA, TANESCO n.k kutafuta namna Bora itakatotumika kufikisha huduma kwenye maeneo ya uwekezaji.
“baraza hili ni halali na muhimu liko kisheria, hivyo sekta binafsi, sekta za umma, tumieni fursa za Baraza la biashara kukuza kipato ukiachilia mbali changamoto zilizopo” Alisema Gowele.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kibiti Mohamed Mavura ambaye ndiye alikuwa Katibu wa Baraza hilo alitangulia kusema ni wakati wa wafanyabiashara na wawekezaji wa Kibiti kuchangamkia fursa zilizopo ikiwa ni sambamba na kuanzisha maghala ya kuhifadhia mazao na vinu vya kukobolea kwani katika ngazi ya Wilaya kuna matarajio makubwa ya kuvuna mazao mengi hususani katika zao la mpunga .
“Tuna hekari zipatazo 8500 za mpunga zimelimwa tunatarajia kuvunja Kiasi kikubwa cha mazao” alisema Mavura.
Kutokana na uwekezaji huo Mavura amesema Serikali kupitia ngazi ya Wilaya inapambana kutafuta maeneo Kwa ajili ya uwekezaji na wakati huo huo akaisisitiza Taasisi ya Tanesco kwenda mkupuka kuona namna ya kuweza kufikishwa umeme katika eneo hilo la Viwanda .
Vilevile Kwa upande wa yatokanayo na kikao kilichopita kuhusu uwekezaji maagizo yamezingatiwa hususani upande wa uwekezaji Halmashauri imekwisha bainisha maeneo ya uwekezaji katika Kijiji cha Mkupuka hekari 25 na hekari 5533 katika Kijiji cha Muyuyu kwa ajili ya uwekezaji, mazimio mengine yalikuwa ni upandaji wa miti, kusimamia sheria zilizopo n.k yamezingatiwa ipasavyo.
Akielekeza fursa zilizopo kwenye maeneo ya uwekezaji Wilaya ya kibiti Afisa Biashara Sadelick Kihongosi amesema, Kibiti ina fursa nyingi za uwekezaji kama kilimo cha umwagiliaji katika zao la mpunga na miwa, fursa ya kilimo cha Ufuta, chikichi, alizeti, mihogo na matunda. Vilevile amesema kuna fursa ya uwekezaji wa hoteli za kitalii hasa ukanda wa visiwani (delta) katika maeneo ya Jaja, Simbaulanga na Nyamisati. Mbali na fursa hizo pia amesema kuna uwekezaji katika uvuvi na ufugaji wa samaki kwa kutumia mabwawa, unenepeshaji wa ng’ombe na uanzishwaji wa Ranchi za mifugo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibiti Ramadhani Mpendu, amewashukuru wadau wote na wataalamu kushiriki kikao hicho na kusisitiza upendo katika utendaji, huku akisema wadau wapaishe nembo ya kibiti kwa kufanya maendeleo na kuwa wazalendo kwa Wilaya yao,
Aidha baadhi ya wadau kwa nyakati tofauti wameomba kuboreshewa na kurahisisha upatikanaji wa vitendea kazi ambavyo ni changamoto kubwa hususani kwenye Uvuvi, Kwa upande wa nyamisati kuboresha kiwanda kilichopo kwani kinafanya kazi Kwa kusuasua ili kiweze kutoa huduma stahiki kwenye jamii, pia kuhakikisha mtambo wa kuzalisha barafu unakuwa imara.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.