Baraza la Wahe. Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti limeagiza mwekezaji Jenga Tanzania kupewa hekari zote zilizopatikana ili aweze kuanza haraka uwekezaji wa kilimo cha alizeti Wilayani humo.
Mwekezaji huyo aliomba kupatiwa hekari 20,000 kwaajili ya uwekezaji wa Kilimo cha Alizeti na kujenga kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti lakini ardhi iliyopatikana ambayo imetengwa kwaajili ya uwekezaji ni hekari 15,444 pekee. Hivyo Wahe. Madiwani wameridhia Mwekezaji huyo kupewa ardhi hiyo yote.
Hayo yamejiri tarehe 14.6.2024 katika kikao cha Baraza la Madiwani la robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ambapo walikuwa wakijadili taarifa za utekelezaji wa majukumu ya kamati za kudumu kwa robo ya tatu (Januari-Machi, 2024).
Madiwani wote kwa pamoja wameridhia na kuzipitisha taarifa za kamati zote.
Awali akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa Baraza hilo Mhe. Ramadhan Mpendu ametoa pole kwa wananchi wote walioathiriwa na Mafuriko, sambamba na kutoa shukrani kwa Serikali na wadau mbalimbali kwa kuwapatia misaada katika kipindi hicho. Pia ametoa pongezi kwa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kibiti, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti pamoja na watumishi wote kwa namna walivyojitoa kuwasaidia waathirika wa mafuriko Wilayani humo.
Mbali na hayo pia Mhe. Mpendu amewataka wananchi wa Kibiti kuendelea kufanya palizi katika mashamba yao ya Korosho katika kipindi hiki ili kujihakikishia mavuno ya kutosha msimu wa zao hilo ukifika, hata hivyo amewasisitiza wananchi/wakulima wote katika msimu huu wa ufuta kuhakikisha wanapeleka ufuta kwenye maghala yaliyoandaliwa kwa ajili ya Mauzo.
Naye Katibu Tawala Wilaya ya Kibiti Bi. Maria Katemana akitoa Salam za Serikali kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya amesema Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo amewashukuru viongozi wote wa Wilaya kwa namna walivyotoa ushirikiano katika shughuli za Mwenge wa Uhuru na katika janga la Mafuriko ambapo mpaka sasa Kambini zote zimebaki kaya 178 kati ya 436 zilizokumbwa na Mafuriko.
Pia Kanali Kolombo ameipongeza Kamati ya elimu na wadau wa Elimu kwa kuchangia madawati, viti na meza ambapo Leo 14.6.2024 NMB wametoa madawati 100 katika shule ya Msingi Kitundu na kusisitiza zoezi hilo kuwa endelevu. Na katika salamu nyingine amesema, Serikali zimesisitiza kuwepo kwa utaratibu mzuri wa kuwapa maeneo wawekezaji kwa maendeleo ya wa Wilaya.
Aidha Bi. Katemana amesema Mkuu wa Wilaya ameagiza na kusisitiza Idara ya kilimo, Viongozi wa Kata na vijiji kusimamia vizuri zoezi la ugawaji wa mbegu tayari kwa kupandwa hususani kwa wakazi wa delta na waliofikwa na Mafuriko, ambapo mpaka sasa tumekwishapokea tani 5 za mpunga na Tani 3 za mahindi kutoka Wizara ya Kilimo kupitia Wakala wa mbegu Morogoro (ASA).
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.