Baraza la Madiwani Wilaya ya Kibiti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 limekutana katika ukumbi wa Halmashauri kujadili taarifa mbalimbali za robo ya pili na wote kwa pamoja wameridhia na kuzipitisha.
Awali Mkurugenzi Mtendaji Mohamed Mavura ambaye alikuwa Katibu wa baraza hilo akitoa taarifa ya wilaya amesema kumekuwa na wimbi la uuzaji holela wa ardhi hivyo ameandika barua ya zuio la uuzaji wa maeneo hovyo na amewaagiza watendaji wote kusimamia kikamilifu jambo hilo. Kwa upande wamaafa ya hivi karibuni yaliyotokana upepo mkali na mvua zinazoendelea kunyesha amewataka Madiwani kushirikiana na viongozi wa vijiji au kata Pamoja na wananchi kutatua changamoto ndogodogo ambazo zipo ndani ya uwezo wao kuliko kuendelea kusubiri Halmashauri ifanye Kila kitu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kibiti Mhe. Ramadhan Mpendu akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ambaye anashiriki kwa mara ya kwanza katika baraza la madiwani Wilayani Kibiti, amempongeza Mkuu wa wilaya ya Kibiti Kanali Kolombo kwa kuteuliwa na Rais na kuahidi kumpa ushirikiano wa kutosha katika utendaji. Vilevile amepongeza mkuu wa wilaya ya Rufiji aliyekuwa akikaimu kwa muda wa miezi kadhaa kwa kazi nzuri aliyoifanya Wilaya ya Kibiti licha ya kuwa na majukumu mengi.
Katika baraza hilo Mpendu amewasihi viongozi kumuunga mkono Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha watoto wote wanakwenda shule katika ngazi ya msingi na sekondari kwani elimu ni bure na amefanya jitihada nyingi kupunguza kero kwa kujenga shule nyingi karibu na jamii jambo linalowapunguzia safari watoto kutembea mwendo mrefu kwenda shule.
Vilevile Mpendu amesisitiza wananchi wa kibiti kutumia vizuri msimu huu wa mvua kwa kulima mazao ya biashara na chakula wa wingi ili kuweza kuwa na uhakika wa kuwa chakula cha kutosha na siyo kulima mazao ya biashara pekee.
Akitoa salamu za serikali Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amelishukuru baraza la Madiwani kwa mshikikamano na kuwataka kuendelea kudumisha ushirikiano kuhakikisha kibiti inasonga mbele.
Kanali kolombo amewataka madiwani na watendaji wote kuhakikisha wanasimamia vizuri miradi ya maendeleo ili mwenge wa uhuru utakapokaguwa miradi ya maendeleo mwaka huu kusiwe na dosari ya aina yeyote.
“tujiandae mwenge utakagua miradi ya maendeleo tusimamie vizuri ukaguzi usiwe na dosari” Alisema Kanali Kolombo.
Pia Mkuu wa wilaya Kolombo ameagiza watendaji na Madiwani kutambua idadi ya wanyama waliopo kwa makundi ili kuruhusu zoezi la kuanza kugawa maeneo ya vitalu vya kufugia (Ranchi ndogo ndogo) kwa ajili ya wafugaji kuweza kufugia mifugo yao kama serikali ilivyoagiza.
Aidha amewataka Wazazi wa kata ya msala kupeleka watoto katika shule ya nyamisati inayotoa huduma kwa sasa wakati wakisubiri kukamilika kwa ujenzi wa shule mpya katika maeneo na siyo kukaa na watoto majumbani.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya kibiti Juma Ndaruke katika baraza hilo amelitaka shirika la umeme TANESCO kuhakikisha linapata muafaka juu ya tatizo la kukatika Kwa umeme mara kwa mara Pamoja na kuimarisha njia za mapitio ya umeme ikiwa ni pamoja na kukata miti iliyokaribu nan jia za umeme.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.