Baraza la Madiwani Wilaya ya Kibiti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 robo ya tatu, limeketi katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya, kujadili taarifa mbalimbali ambapo kwa pamoja wameridhia na kuzipitisha ajenda mbalimbali.
Awali Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Mohamed Mavura ambaye ndiye Katibu wa baraza hilo, akitoa taarifa ya Halmashauri amesema kwa mwaka huu, kumekuwa na changamoto ya upungufu wa mazao kutokana na mabadiliko ya Hali ya hewa (mvua chache) na kupelekea uzalishaji kuwa mdogo. Hali hiyo pia imesababisha kuvunja/ kuvuruga ratiba za vikao kutokana na kupungua kwa mapato.
Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya kibiti katika baraza la madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mhe. Ramadhan Mpendu, amewataka wakazi wa kibiti kupeleka mazao yao ghalani na kuuza kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani hususani katika zao la UFUTA ambalo kwa sasa ni msimu wa mauzo n.k
Vilevile Mhe. Mpendu amewaelekeza wananchi wa kibiti kujikita katika kilimo Cha mazao ya chakula mbali na mazao ya biashara pekee kwa kuzingatia mabadiliko ya nchi Kwa ujumla (uchache wa mvua).
" wanakibiti limeni mazao ya biashara na chakula kwa wingi ili kuweza kuwa na uhakika wa kuwa na chakula cha kutosha na siyo kulima mazao ya biashara pekee". Alisema Mhe. Mpendu.
"Mhe. Mkuu wa Wilaya kwa Mamlaka uliyo nayo naomba tusaidie kuweka msisitizo kwa wananchi kuhakikisha wanalima mazao ya chakula kila msimu ili kusiwepo na ukosefu wa chakula ndani ya Wilaya" Alisema Mhe. Mpendu.
Aidha amemwomba Mkuu wa Wilaya Pamoja na viongozi wengine kupiga marufuku uchezaji holela wa michezo ya bahati nasibu (betting) au michezo ya jamii ya kamali kwa kuzingatia umri na kutocheza michezo hiyo mida ya kazi ili kuwa na kizazi watu wakafanye kazi za kimaendeleo na kujikwamua kiuchumi.
Mbali na hayo, Mwenyekiti Mpendu amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi anazotoa kutekeleza miradi ya Maendeleo katika Wilaya ya Kibiti na Tanzania kwa ujumla. Licha ya kongole hizo amewapongeza Viongozi wote katika ngazi ya mkoa na wilaya kwa namna wanavyosimamia miradi na kukamilika kwa wakati.
Katika barazani hilo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo akiwa amembatana na Kamati ya Ulinzi na usalama amelipongeza barazani la Madiwani, Viongozi na watumishi wote kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru na kuipatia Wilaya sifa nzuri.
" Nilifarijika sana kwa umoja na ushirikiano wenu, endelezeni ushirikiano huo tuijenge Kibiti yetu, kwa maendeleo yetu kwani sisi ni familia moja" Alisema Kanali Kolombo.
Akijibu maoni ya taarifa ya Mwenyekiti wa Halmashauri Halmashauri kuhusu kuhamasisha ulimaji wa mazao ya chakula, Kanali Kolombo amesema amelibeba suala hilo na katika msimu ujao atasimamia kikamilifu kuhakikisha mazao ya chakula yanalimwa kwa wingi na kupata chakula cha kutosha na si kulima mazao ya biashara pekee. Hata hivyo katika msimu huu wa ufuta ameagiza uongozi na wananchi kwa ujumla kuhakikisha ufuta hautorishwi na kuuza nje ya Wilaya ya Kibiti.
"Uzeni ututa wenu ndani ya Wilaya yetu wenyewe, wakulima acheni tabia ya kutorosha na kuuza ufuta nje, tunawafaidisha wenzetu kimaendeleo, kuweni wazalendo tuijenge Kibiti yetu" Alisema Kanali Kolombo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kibiti Mhe. Twaha Mpembenwe akiwa katika baraza la madiwani mara baada ya mjadala amesema, amepokea changamoto Pamoja na maoni yote, Pia Mpembenwe amesema kwamba Bunge la bajeti linaendelea tarajieni kupata miradi mipya na mpaka sasa tayari tumeshapokea pesa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Kibiti katika Kijiji cha Nyambili, hivyo endeleeni kuniamini Mbunge wenu niko kazini nawapambania.
Kwa upande wa kilimo Cha umwagiliaji Kibiti Mhe. Mpembenwe amesema kuhusu masuala ya banio la maji ambalo ni suluhisho la kilimo hicho Wilaya ya Kibiti, amekwisha zungumza na Waziri wa kilimo na tayari tume ya umwagiliaji imekwisha wasili kwa ajili ya upembuzi yakinifu wakati mazungumzo yakiendelea.
Vilevile Mhe. Mpembenwe amemtaka Mkurugenzi kuongeza nguvu kwenye usimamizi wa vyanzo vya mapato kwa kushirikiana na wananchi kwa ujumla jambo litakalotusaidia kujua njia za panya zinazosabisha mapato kupotea na kuzidhibiti kikamilifu.
Kwa upande wa elimu Mhe. Mbunge amesema suala la ufaulu wa watoto mashuleni ni jukumu la Viongozi wote wakiwemo madiwani hivyo, kuna kila sababu ya kukaa kutafuta mikakati madhubuti itakayowezesha watoto kufanya vizuri madarasani, huku akiwapongeza Viongozi wote kwa kazi nzuri wanazozifanya kuhakikisha Kibiti inasonga mbele kimaendeleo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.