Wakulima wa mbaazi Mkoa wa Pwani wameonekana kufurahishwa na kupata matumaini ya bei ya zao hilo ambalo kimauzo lilikuwa chini zaidi ukilinganisha na mazao ya Korosho na Ufuta.
Hayo yamejiri katika Mnada wa pili wa zao la mbaazi Mkoa wa Pwani ambao umefanyika tarehe 13.09.2024 Wilayani Kibiti. Katika mnada huo Kibiti imefanikiwa kuuza jumla ya Tani 19 na kg 667 kati ya Tani 122 na kg769 zilizouzwa kwa Mkoa mzima baada ya wakulima wote kuridhia kwa pamoja.
Baada ya kuchakata bei katika mnada huo, mbaazi zimeuzwa kwa bei ya wastani ya sh 1753.88 kwa kilo ambapo bei ya juu ilikuwa Sh.1760 na bei ya chini Sh.1750.
Mara baada ya mnada huo kumalizika Meneja wa CORECU Mkoa wa Pwani Ndg. Hamis Mantawela ametoa rai kwa wakulima wa mbaazi Mkoani humo kulichukulia zao hilo mbadala la kibiashara kuwa fursa kwa kuhakikisha wanakuwa na mbaazi bora zilizokauka vizuri.
Vilevile Bw. Mantawela amewataka wakulima ambao bado wanavuna kuongeza kasi zaidi na kufikisha mapema mazao yao ghalani hususani wakati huu ambao bei bado ni nzuri.
Aidha Mwakilishi wa wakulima wa mbaazi Ndg.Kassim Juma amesema kwa mwenendo wanaouona wa bei ya mbaazi kwa kilo wamefarijika na kufurahishwa sana kwani mnada umeleta matumaini, walizoea kuuza zao hilo kwa bei ya chini ambapo kwa wastani walikuwa wakiuza Sh. 200-300 kwa kilo.
Hata hivyo Ndg. Kassim amesema anatumaini mnada ujao wakulima wataongezeka kwa kasi zaidi lakini pia amewataka wakulima wenzake kuandaa mbegu bora mapema kwa ajili ya msimu ujao huku akisisitiza kutenga maeneo kwa ajili ya kilimo hicho.
"Wakulima wenzangu hii ni fursa, kama kuna mkulima analima ekari 20 za ufuta au korosho, basi atenge angalau eka 4 kwa ajili ya Kilimo cha mbaazi" Alisema.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.