Tukiwa katika kipindi cha kudhibiti mikorosho kwa ajili ya msimu mpya Bodi ya korosho imekutana na Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya kibiti kutoa uelewa na mwongozo wa usambazaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa Korosho nchini msimu wa 2023/24 Kwa mfumo wa kidigitali.
"Tumeona kabla ya zoezi kuanza tuonane na Kamati ya ulinzi na usalama, ili tuwape uelewa wa usambazaji, mtusaidie kudhibiti pembejeo panapokuwa/ panapotokea viashiria vya uchepushaji wa pembejeo" Alisema Mkangara.
Akiwa katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri Mkurugenzi Msaidizi tawi la Dar es salaam Bi Domina Mkangara akimwalilisha Mkurugenzi wa bodi ya korosho Tanzania amesema, kupitia mfumo huo kila mkulima aliyejisajili atapata pembejeo zake zote kwa pamoja kama alivyojisajili kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mkulima anapata kinachostahili kulingana na idadi ya miti ya mikorosho aliyoorodhesha.
"Kila mkulima atapata pembejeo kupitia idadi ya miti aliyoorodhesha kwenye shamba lake" Alisema Mkangara.
Vilevile Bi Mkangara amesema kwa mwaka wa msimu wa 2023/24 malengo ya Serikali ni kuzalisha Tani 400,000 na tani 700,000 ifikapo mwaka 2025/26 za korosho hivyo Kuna kila sababu ya kuongeza tija kwa kutoa pembejeo ambapo wakulima wadogo wataweza kuhudumia mikorosho yao kwa asilimia 100% na wakubwa asilimia 66% kwa kuweza kupuliza miti 4 kati ya 6.
"Serikali imeamua kuwapunguzia makali wakulima wadogo kwa 100a% na kwa wakulima wakubwa kwa 66% kulingana na utaratibu wa ugawaji wa ruzuku"Alisema Mkangara.
Akielekeza namna ya kutumia mfumo huo wa kidigitali Bi Mkangara amesema, kila mkulima aliyejisajili atapewa namba yake ya Siri itakayomsaidia kuingia kwenye mfumo kupitia Viongozi wa Amcos, ambao tayari wamekwishapewa mafunzo kuweza kutumia App maalum iliyoandaliwa ambayo itaonyesha anachostaili kulingana na idadi ya miti aliyoainisha wakati wa usajili.
Hata hivyo Afisa kilimo Wilaya ya Kibiti ameipongeza bodi kwa kuanzisha mfumo huo huku akisisitiza kuhakikisha majina ya waliosajiliwa yanabandikwa mapema ili waliochaguliwa kujitambua mapema na kufuata taratibu stahiki kwa usahihi kama vile kuwa na vitambulisho,lessen au barua kutoka kwa Mwenyekiti wa Kitongoji itakayomtambulisha.
Aidha akifunga kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amewapongeza Wataalam kwa wasilisho zuri la kitaalam huku akiwaagiza kuhakikisha zoezi hilo linaanza mapema ili kupunguza na kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza wakati zoezi likiendelea .
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.