22.3.2024.
Baada ya kuonekana kuwepo kwa taarifa zisizo na uwazi katika usajili na uchukuaji wa pembejeo kidigital, Bodi ya Korosho imeendesha mafunzo ya usajili wa pembejeo kwa wakulima kwa lengo la kuhuisha taarifa zao (data) , kuweza kupata takwimu zinazotambua ukubwa wa mashamba na idadi ya miti iliyopo shambani.
Akiendesha mafunzo hayo Afisa Tehama wa Bodi ya korosho Ndg. Gerald Rogathe amesema mafunzo hayo yatawasaidia kupata kanzidata za wakulima wote wa korosho Wilayani Kibiti kwa haraka huku wakitarajia kuwa itakuwa ni njia nzuri ya kupata taarifa sahihi za mashamba , mikorosho na wakulima kwa ujumla.
Afisa huyo amesema, usajili unaofanywa sasa kwa njia ya kidigitali utawasaidia kufanya maandalizi ya ugawaji wa pembejeo tayari kwa kuanza kwa msimu mpya wa kilimo kwa mwaka 2023/2024 ambapo wamejipanga kuanza zoezi hilo mwishoni mwa mwezi wa nne mwaka huu.
Aidha Afisa Kilimo Ndg. Mrisho Mnobwe amewasisitiza maafisa ugani kujitahidi sana kuhakikisha kazi zinafanyika kama ilivyoelekezwa na kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati tayari kwa kuanza maandalizi ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuanza upuliziaji wa miti ya mikorosho.
Upande wao mabwana shamba (maafisa ugani) wamesema, mafunzo hayo yatawasaidia kusimamia zoezi la makarani liweze kwenda vizuri na kupeleka taarifa sahihi ngazi ya Wilaya, wakati Makarani wakisema yamewasaidia kuelewa namna ya kusajili wakulima wa korosho na kuwaweka kwenye mfumo ili waweze kutambua takwimu zilizo sahihi kwa urahisi.
Mafunzo hayo yamehusisha maafisa ugani na Makarani watatu kutoka katika kila Kijiji.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.