30.5.2024
Bodi ya Shule, wakiwemo Walimu, Wazazi, Watumishi mbalimbali na Serikali ya Wanafunzi wa Shule ya Wavulana Kibiti wamemkabidhi Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibiti Bi. Maria Katemana msaada wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya waathirika wa mafuriko Wilayani humo.
Vifaa vilivyotolewa ni matunda, mbogamboga, unga, pampasi, majani ya chai, sabuni ya mche ,mafuta ya kupaka na mchele.
Kabla ya Katibu Tawala kupokea msaada huo Mwenyekiti wa Bodi hiyo ya shule Bw. Dotto Mandago alisema msaada huo unakuja baada ya kuguswa na maafa yaliyotokea Wilaya ya Kibiti kutokana na Mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha nchini.
Hata hivyo katika makabidhiano hayo Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibiti Mwl. Lawrence Mwakyoma amefafanua kwamba, vifaa hivyo vinatokana na michango yao binafsi kwa umoja wao ikiwa ni sehemu ya kutoa pole kwa wahanga hao.
Kwa niaba ya Serikali ya Wanafunzi Kaka Mkuu Robert Martine Giles amesema wameona watoe sadaka hiyo ili ndugu zao nao wakapate faraja na kutambua kuwa jamii inayowazunguka inawakumbuka.
Vilevile Afisa Elimu Divisheni ya Awali na Msingi Mwl. Zakayo Mlenduka ameishukuru Bodi hiyo kwa misaada walioitoa huku akisema kwamba vifaa vilivyopokelewa ni msaada mkubwa kwa waathirika hao, ambapo wameelekeza vipelekwe shule ya Msingi Kitundu walipo wanafunzi wa darasa la 4 na la 7 ambao wamewekwa kambi kuendelea na masomo, ili waweze kuendelea na maandalizi ya mitihani yao ya Taifa.
Akipokea vifaa hivyo Katibu Tawala kipekee amewashukuru Viongozi shule hiyo kwa moyo wa upendo kwani pamoja na kutoa msaada huo tangu awali walitoa chumba kimoja kutumia kama ghala kuu kwa ajili ya kupokelea misaada kabla ya kusambazwa kwa waathirika.
"Kipekee tunawashukuru sana kwa niaba ya Serikali, vifaa vilivyotolewa vinakwenda kugusa Afya na mahitaji ya walengwa Moja kwa Moja nitahakikisha vinawafikia kama mlivyokusudia" Alisema Bi. Katemana.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.