.
MKUU wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amekutana na wananchi wa Kata ya Mtunda katika kikao maalum kusikiliza, kujadili na kutatua kero za matukio mbalimbali zinazotokea katika Kata hiyo ikiwa ni pamoja na suala la wafugaji.
Akiwa katika Kijiji cha Mtunda B ambako mkutano huo umefanyika, Kanali Kolombo, amewataka wafugaji wa Kata ya Mtunda kuishi kwa kufuata sheria taratibu na kanuni za vijiji na vitongoji wanavyoishi wakiwa na mifugo yao kwa amani bila kuleta migogoro.
"Suala la kuhamisha wafugaji ni gumu, nitawapeleka wapi? Kikubwa wafugaji fuateni sheria na taratibu zilizopo muishi Kwa amani, Sina pa kuwapeleka" Alisema Kolombo.
Vile vile amesema kutokana na mrundikano wa malalamiko ya kesi takribani 28 mahakani, Kanali Kolombo ameagiza kuanzishwa kwa Mahakama inayohama katika Jengo la Mahakama ya Kikale ndani ya Kata hiyo ili iweze kupunguza kesi zilizopo Kwa wakati na kuwapunguzia mwendo mrefu wakazi hao ambao hutegemea Mahakama ya Kibiti.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amepiga marufuku kitendo cha kutembea na silaha mitaani ikiwa ni pamoja na marufuku ya kuachia ng'ombe usiku katika mashamba ya watu.
Aidha Kanali Kolombo amewataka wakazi wote wa Mtunda na vitongoji vyake kutoa ushirikiano na kulipokea zoezi la uanzishwaji wa ranchi ndogo za wafugaji (vitalu) ambao unakwenda kuwa suluhisho la malumbano ya wakulima na wafugaji.
" Uanzishwaji wa ranchi ni suluhisho la migogoro kati ya wafugaji na wakulima lipokeeni, hii itawajengea na kurejesha mahusiano mazuri ambayo yamelegalega Kwa muda mrefu "Alisema Kolombo.
katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya aliambatana na Kamati ya ulinzi na usalama pamoja na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kutoka idara ya mifugo, Ardhi, pamoja na Uongozi wa Mkoa unaoendesha zoezi hilo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.