February 5, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amekabidhi mabati 120 kwa ajili ya kuezeka boma la nyumba ya mwalimu katika Kijiji cha Nyanjati Kata ya Mahege, ikiwa ni sehemu ya kutimiza ahadi yake ya kuwapatia mabati 80 aliyoitoa tarehe 29/01/2024.
"Leo nimetimiza ahadi yangu,Serikali yenu iko makini, ni sikivu na inawajali, na leo tunakabidhi mabati 120 na siyo 80 tena kama nilivyoahidi Awali, sasa kazi iendelee" Alisema Kanali Kolombo.
Mara baada ya kukabidhi mabati hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kibiti Ndg. Hemed Magaro alisema kuwa, kabla ya kuleta mabati hayo walifanya upembuzi yakinifu na Mhandisi wa majengo na kubaini jumla ya mabati yanayotakiwa ni 148.
"Tulifanya tathmini na kubaini boma linahitaji mabati 148, tumekabidi 120 hivyo bado tuna upungufu wa mabati 28 na yatakuja". Alisema Magaro.
Vilevile Mkurugenzi Magaro amesema kwa upande wa boma la nyumba ya Mganga (Afya) tayari limekwishaingizwa kwenye mpango na jengo la utawala litasubiri bajeti ijayo na litakamilika kwa kadri bajeti itakavyoruhusu.
Aidha Mkuu wa Taasisi ya kupambana na rushwa Wilaya ya Kibiti Bi Anna Shine amewataka wakazi wa Kijiji cha Nyanjati kuhakikisha mabati waliyokabidhiwa yanafanya kazi iliyokusudiwa na si vinginevyo.
"Hiyo ni fedha ya Serikali, mkayatumie mabati haya kama inavyotakiwa" Alisema Bi Anna kwa msisitizo.
Mwisho Viongozi wa Kata hiyo wamewashukuru viongozi wote wa Halmashauri, kwa kufanya kazi kwa vitendo na kudai kwamba upokeji wa mabati hayo utawafanya watembee kifua mbele kwa wananchi wakiwa na neno la kusema na sasa hata wakiitisha vikao ,wananchi wataitikia wito.
Awali wajumbe (Viongozi) hao waligoma kuendelea kushiriki vikao vya aina yeyote kijijini hapo mpaka wajue hatma ya ukamilishaji wa maboma hayo kwani yalifanya waonekane wababaishaji kwenye jamii.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.