Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ametoa wiki 2 kwa RUWASA Wilaya ya Kibiti kuhakikisha wanatatua kero za wananchi zinazohusiana na maji.
"Ninawapa wiki mbili kuhakikisha kero za Wananchi zinazohusiana na maji mmezipatia ufumbuzi, watu wanahitaji maji na sio maneno, nendeni mkawasililize msikae ofisini" Alisema.
Hayo yamejiri katika Mkutano Mkuu wa pili wa wadau wa sekta ya maji vijijini na wakala wa Maji na usafi wa Mazingira vijijini uliofanyika tarehe 24.06.2024 katika ukumbi wa shule ya Sekondari ya wavulana Kibiti.
Akifungua mkutano huo Kanali Kolombo alimpongeza Mhe. Rais Dkt. SSH kwa kutoa fedha za miradi ya maji kibiti. Pia alieleza kuwa lengo la mkutano huo ni kutathmini hali ya maji, kuweza kutambua changamoto zolizopo na kuboresha mapungufu ili miradi hiyo iweze kuwa endelevu kwa kutoa maji muda mrefu.
Hata hivyo mewaagiza Viongozi kuhakikisha wanasimamia vizuri miradi ya maji ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi wa miundombinu hiyo huku akiwashukuru wajumbe na wadau hao wa maji kwa kushiriki mkutano huo.
Mkutano huo ulioongozwa na Mkuu wa wilaya ulishirikisha wadau mbalimbali wa maji wakiwemo Madiwani, watendaji wa Kata, watendaji wa vijiji, wenyeviti wa vijiji na Vitongoji ambao pia waliweza kuelezea kero za wananchi kuhusu maji.
Katika mkutano huo Makamu Mwenyekiti wa baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mhe. Omari Twanga amewataka RUWASA na watendaji wengine wa Serikali kuendelea kushirikiana kwa dhati kwa kuibua changamoto zilizopo na kuzipatia suluhisho ili kuweza kutimiza lengo la Serikali ya kila mwananchi kupata maji safi na salama katika maeneo ya karibu.
Aidha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Denis Kitali aliwataka RUWASA kukabiliana na changamoto zolizopo kwa kuzipatia ufumbuzi kwani suala la maji linamgusa kila mtu na kazi kubwa ya Serikali ni kutekeleza ilani iliyopo madarakani kwa kuwahudumia wananchi.
Naye Kaimu Meneja wa RUWASA Kibiti Mhandisi Juma Ndaro Alisema ngazi ya Wilaya wameweka mikakati kabambe ikiwa ni pamoja na mpango wa kuhakikisha wanafikia 85% usambazaji wa maji kwa kuibua miradi mipya ya maji na kukarabati ya zamani.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.