24.06.2024
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo akiwa pamoja na Kamati ya Ulinzi na usalama amefika katika Kijiji cha Nyamisati na kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa waathirika waliounguliwa nyumba zao tarehe 9 juni na kusababisha kifo cha mtoto wa miezi 6 katika Kijiji cha Mfisini na msaada mwingine kuelekezwa Shule ya Sekondari Nyamisati.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ofisi ya Mtendaji Kata ya Salale ambapo Kanali Kolombo alieleza kuwa ameikabidhi familia ya bwana Juma Ngwachi na familia ya bwana Sultani Kigomba vifaa vyenye jumla ifuatayo: Unga kg 30, mchele kg 50 , mablanketi pisi 5, shuka pisi 5, ndoo kubwa za maji 10 zenye ujazo wa lita 20, mabeseni ya plastiki 3, mafuta ya kupikia lita 10 , magodoro 7, maharage kg 15.
Mbali ya misaada hiyo pia ameikabidhi shule ya Sekondari Nyamisati magodoro 50 pamoja na mabalo 2 yenye blanketi 100 kwa ajili ya kusaidia watoto wanaoweka kambi kwa lengo la kujiimarisha kupandisha ufaulu mashuleni.
Mara baada ya makabidhiano Katibu wa Siasa na Uenezi CCM Kata ya Salale Bi.Amina Juma ameishukuru Serikali na Viongozi wote wa Wilaya kwa kuwakimbilia na kuwapa mkono wa pole waathirika hao ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala.
Aidha wawakilishi wa familia hizo zilizopata madhara kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali kwa kuwajali kwani wamefarijika sana.
Pia Mwenyekiti wa Bodi ya Shule baada ya kupokea msaada kwa ajili ya wanafunzi ameahidi kuwa watafanya jitihada za hali na mali kupandisha ufaulu kwani sasa suala la malazi kwa watoto halina kisingizio kwakuwa wamepata magodoro.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.