NI KATIKA KIKAO CHA KAMATI YA AFYA MSINGI.
Katika kuhakikisha chanjo mbalimbali zinawafikia wananchi nchini Wizara ya Afya Ofisi ya Rais Tamisemi imeandaa kampeni ya kitaifa ya kutoa chanjo ya Surua na Rubella kwa watoto wote walio na umri wa miezi 9 mpaka chini ya miaka 5 kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo. Kampeni hii itaanza tarehe 15/02/2024 hadi 18/02/2024.
"Lengo la kampeni hii ni kuongeza Kinga kwa walengwa kwa kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Surua na Rubella kwa watoto wote bila kujali kuna aliyekwishapata chanjo Awali au la" Alisema Frank Patrick Mratibu wa chanjo Wilaya ya Kibiti.
Katika kikao hicho Mratibu huyo amesema mkakati wa utoaji wa chanjo utahusisha vituo vya kudumu vya kutolea huduma za Afya, huduma za mkoba na kliniki tembezi kwa vituo na vituo vya kuhamahama vitakavyopangwa. Vilevile amesema utoaji wa chanjo hizo utatekelezwa katika maeneo mbalimbali kama vile sokoni, shuleni, nyumba za Ibada, vituo vya mabasi, kambi za wavuvi, wakimbizi ,vituo vya mipakani na popote penye watoto.
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya Daktari Elizabeth Oming'o amesema ni muhimu kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo hususani watoto wa kike kwani madhara ya magonjwa hayo ni makubwa yakipuuzwa ikiwa ni pamoja hapo baadaye kuzaa mtoto aliyefia tumboni, kiziwi, mlemavu, kuzaa mtoto mwenye moyo wenye tundu na hata kusababisha vifo kwa sababu mara nyingi huambatana na homa Kali.
Akizindua kampeni hiyo Mkuu wa wilaya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amesema utoaji wa chanjo utasaidia kuzuia kuenea kwa magonjwa hayo. Hivyo amewataka wazazi na walezi wote wenye watoto wenye umri uliotajwa kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kupata chanjo.
Mara baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo, Kanali Kolombo ameiagiza Idara ya Afya kutoa matangazo na kutengeneza vipeperushi vinavyoeleza umuhimu wa chanjo hiyo haraka na Vituo vitakavyohusishwa na kuvisambaza sehemu mbalimbali ili jamii ipate kutambua ni zoezi linaloendekea nchini.
"Zoezi hili linafanyika nchi nzima, sambazeni taarifa haraka ili kurahisisha kampeni hii kufanyika kwa wakati uliopangwa" Alisema Kanali Kolombo.
Mbali na agizo hilo amewataka wananchi wote kuwa mabalozi wa chanjo kwa kuhakikisha kila anayepata ama kusikia tangazo hilo linalohusu Chanjo basi anamjulisha mwenzake kupeleka mtoto wake kwenda kupata chanjo kwani Surua na Rubella ni magonjwa yanayoweza kukingwa kwa njia ya chanjo hivyo yasipuuzwe.
Aidha ametoa angalizo la ujumbe muhimu kwa wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa haraka juu ya madhara atakayopata mtoto baada ya kupewa chanjo au kuona mgonjwa mwenye dalili za homa na vipele kooni na mwilini.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.