Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hanan Bafagih amesema amekuja Kibiti kuendeleza mazuri yote aliyoyakuta kwenye kituo chake hicho kipya ili kuipeleka Kibiti mbele zaidi.
Mkurugenzi huyo ameyasema hayo Agosti 10, 2024 kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi baina yake na mtangulizi wake Ndg. Hemed Magaro ambaye kwasasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilwa.
Akiongea na timu ya menejimenti ya Halmashauri Bi. Hanan ameshukuru sana kwa mapokezi mazuri huku akiomba ushirikiano wa dhati kutoka kwa Watumishi kwa namna ile ile waliyoshirikiana na mtangulizi wake ili kuiendeleza Kibiti.
Aidha Mkurugenzi amebainisha wazi kuwa vipaumbele vyake Kibiti ni viwili navyo ni Kumailizia Miradi ambayo haijakamilika ili ianze kufanya kazi pamoja na Kuongeza mapato ya Halmashauri.
“Ndugu watumishi wenzangu mimi nina vipaumbele viwili, cha kwanza ni kumalizia miradi yote ambayo haijakamilika hata kama hatuna hela tutaomba huko Serikalini lakini kipaumbele changu cha pili ni Mapato. Mimi ni mdau sana wa mapato kwakuwa naamini ili mambo yaende ni lazima tuwe na hela na hilo tutafanikisha kwa kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato, Kibiti tunao uwezo wa kukusanya hata Bilioni 3” Alisema Ndg. Hanan.
Akizungumza kwa niaba ya Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Ramadhani Mpendu amesema Waheshimiwa Madiwani wanamkaribisha sana Mkurugenzi Hanan, na wanaimani kubwa na yeye kwamba anakwenda kuipeleka Kibiti mbele zaidi.
Baraza la Madiwani, Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti wanamkaribisha sana Mkurugenzi huyo na kumtakia heri katika kazi zake ndani ya Kibiti.
Habari picha ni makabidhiano ya Ofisi kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilwa Ndg. Hemed Magaro na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hanan Bafagih yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.