3.4.2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg Hemed Magaro na Wataalam wake wamefanya ziara ya kawaida kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo katika Kata ya Dimani na Kibiti.
Kati ya miradi iliyokaguliwa ni pamoja na Ujenzi wa chumba kimoja cha darasa shule ya Sekondari Dimani chenye thamani ya sh. 26,000,000 ambacho kimekamilika pamoja na choo chenye thamani ya sh 4,000,000 ambacho Ujenzi wake upo katika hatua ya kupandishwa ukuta huku shimo la choo hicho likiwa limeshachimbwa na ujenzi ukitarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.
Vilevile wamekagua Ujenzi wa matundu matano ya choo pamoja na shimo la maji taka vyenye thamani ya sh 6,600,000 katika shule ya Msingi kimbuga. Ujenzi wa choo hicho upo katika hatua ya linter.
Hawakuishia hapo pia wamekagua Ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na viwili vya Ofisi katika shule ya Sekondari ya Wananchi ambavyo mpaka sasa vimefikia usawa wa linter ujenzi huo ni nguvu za wananchi. Pia Halmashauri imepokea Tsh. Milioni mia nne (400,000,000/=) ambapo Milioni 50 ni za umaliziaji wa vyumba vinne vya madarasa na Ofisi mbili, na Milioni 350 ni za ujenzi wa madarasa, jengo la utawala, vyoo, maabara tatu pamoja na mfumo wa maji.
Mbali na kazi hizo pia wamekagua Ujenzi wa choo cha matundu manne katika shule ya Msingi Nyamakonge wenye thamani ya sh 7,200,000 chini ya mradi wa EP4R ambao umekamilika licha ya kuwepo kwa kasoro ndogo ndogo.
Hata hivyo wamekagua Ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi ambao upo katika hatua ya umaliziaji sambamba na ukaguzi wa ujenzi wa jengo la makao makuu ya Wilaya ambapo Ujenzi unaendelea.
Mara baada ya kukagua na kujionea hali halisi, Mkurugenzi Magaro amewaagiza Muhandisi (W), Wasimamizi wa ujenzi na Mafundi kuhakikisha wanakamilisha majenzi yote kwa wakati uliokusudiwa hususani katika Sekondari ya Dimani, kufanya tathmini ya gharama za kumalizia Ujenzi wa choo shule ya Msingi kimbuga na kuziwasilisha wilayani.
Pia katika shule ya Sekondari ya Wananchi amekagua maandalizi ya ujenzi na kuagiza ujenzi huo kuanza mara moja kwani fedha zipo tayari, na kwa Shule ya Msingi Nyamakonge ameelekeza kuhakikisha wanarekebisha kasoro zote zilizoonekana.
Aidha Mkurugenzi amemuagiza Muhandisi wa Wilaya kutengeneza BOQ zenye uhalisia na kusimamia vyema mpango kazi wa Mkandarasi anayejenga jengo la makao makuu ya Wilaya.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.