Tarehe 6.12.2023 Mnada wa nne katika msimu wa korosho Mkoa wa Pwani ulifanyika wilayani Kibiti ukiwa na wazabuni wannne licha ya suala la changamoto ya unyevu kuendelea kuwatesa wakulima kutokana na mvua zinazoendelea.
Katika mnada huo jumla ya Kg. 234,990 za korosho daraja la kwanza zimeuzwa kwa bei ya wastani ya sh 1,506.25 na Kg. 375,906 za daraja la pili zikiuzwa kwa bei ya wastani ya sh. 1,166.41 baada ya kuchakatwa na wakulima wote kuridhia kuuza.
Katika minada yote mpaka sasa Wilaya ya Kibiti imeonekana kuwa kinara wa kuuza Tani nyingi zaidi ikilinganishwa na Wilaya nyingine ambapo kwa siku hiyo pekee wameuza Kg. 415, 867, Mkuranga Kg. 165,358 na Rufiji ikiuza Kg. 6153.
Mbali na kufanyika kwa mnada huo, Meneja wa Corecu Mkoa wa Pwani Ndg, Hamis Mantawela amewasisitiza wakulima na viongozi wa AMCOS kujitahidi kuhakikisha korosho zote zimechambuliwa na kuanikwa vizuri kabla ya kufikishwa ghalani kwani korosho mbovu hupoteza ubora wake sokoni.
"Mpaka sasa hatujapokea mamalamiko yeyote, tujitahidi tusiingize korosho ambazo hazina ubora tafuteni kipima unyevu mpime kabla ya kufikisha ghala kuu." Alisema Mantawela huku akifafanua kuwa changamoto ya unyevu inajulikana kote.
Naye Meneja wa Bodi ya korosho inayosimamia Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam Bi. Domina Mkangara amesema pamoja na changamoto ya hali ya hewa makusanyo ya korosho bado yanaendelea na wakulima wanajitahidi kuzingatia ubora kuhakikisha hawapotezi masoko.
Bi Mkangara amesema wanaendelea kuwaasa wakulima kuhakikisha wanaanika korosho zao pindi hali ya jua inapokuwepo ili viwango vya ubora viendelee kuwepo. Pia amewasisitiza wanunuzi kuendelea kujitokeza kwani korosho bado zipo katika kiwango kizuri.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.