Wajumbe wa Halmashauri Kuu Wilaya ya Kibiti wamepokea na kuridhia utekelezaji wa ILANI ya Chama cha Mapinduzi CCM katika kipindi cha mwaka wa fedha kuanzia julai 2022 hadi disemba 2022.
Hayo yamejiri katika kikao cha Halmashauri Kuu CCM ngazi ya Wilaya kwa lengo la kusomewa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya kibiti.
Akisoma taarifa ya utekelezaji, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amesema Halmashauri imepanga kutekeleza Miradi mbalimbali ya maendeleo yenye jumla ya sh 8,841,173,508,00 ambapo kati ya fedha hizo sh 774,186,508,00 zinatokana na mapato ya ndani ya halmashauri, sh 4,409,177,000.00 fedha za serikali Kuu na sh 3,687,810,000,00 zikitoka kwa wahisani.
Vilevile Kanali Kolombo amesema kuwa, hadi kufikia Disema 31 mwaka 2022 Halmashauri ilipokea jumla ya sh 4,188,884,239.20 sawa na 47.38% ambazo zimepangwa kutekeleza miradi mbalimbali na mpaka sasa jumla ya sh 3,030,016,969,00 ambazo ni sawa na 72%.33 zimetumika kutekeleza miradi ya Maendeleo inayoendelea kutekelezwa na iliyokwisha kutekelezwa.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya amesema katika kufikia malengo, mafanikio ya Wilaya ya Kibiti ni matokeo ya vipaumbele vilivyowekwa kwenye MPANGO wa Maendeleo kwa lengo la kuendeleza na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika sekta za Afya, elimu, kilim, mifugo na ushirika, maji, barabara na mendeleo ya jamii kwa kushirikisha Wadau mbalimbali kama Koffih,Tasaf, Benki ya Dunia, TFS na NGO’S.
Akijibu hoja za wajumbe Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, ndg. Mohamed Mavura amesema kuwa, pamoja na kazi kubwa iliyofanyika Kibiti lakini yapo mapungufu madogo madogo yaliyojitokeza wakati wa ukamilishaji wa kazi hizo hivyo Mavura amewataka Wataalamu wote kila mmoja kwa nafasi yake, asimamie vizuri kazi zake ili kuhakikisha kazi zinafanyika bila mapungufu hata hayo madogo madogo na kuhakikisha Kibiti inakuwa ya mfano wa kuigwa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo na ustawi wa watu wake.
Aidha Mbunge wa Wilaya ya Kibiti Mhe. Twaha Mpembenwe amemtaka Mkurugenzi Mohamed Mavura kuongeza vyanzo vipya vya mapato kuhakikisha kibiti inapata mapato ya kutosha hususani katika maeneo ya visiwani (Delta) ambako kuna mazao ya hewa ya ukaa, mikoko n.k. Vilevile amewataka Madiwani, Mkurugenzi kufuatilia fedha za mfuko wa Jimbo kujua mapato na matumizi na namna zinavyotolewa.
Katika kikao hicho Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya kibiti Mhe. Juma Ndaruke amewataka wataalamu kutumia Taaluma zao vizuri, kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Kawajibikeni ipasavyo, kila mmoja atimize majukumu yake kulingana na nafasi yake, hii itatusaidia kufika mahali tunapotaka kufika.” Alisema Ndaruke .
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibiti Mhe. Ramadhan Mpendu amewataka wajumbe wa Halmashauri kuu kusimamia na kuilinda miradi ya Maendeleo kwa weledi kwani imebeba mabilioni ya fedha za walipa kodi wa Tanzania.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.