14/04/2023
Afisa Elimu divisheni ya Awali na Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Mwl. Zakayo Mlenduka ambaye ndiye Mwenyekiti wa Miradi mbalimbali inayotekelezwa Wilayani humo akiambatana na Wasaidizi wake Pamoja na Mhandisi, wamefanya ziara ya ukaguzi wa maeneo yatakapojengwa majengo mpya ya madarasa kwa Shule za Msingi na nyumba za walimu katika Kata za Mtawanya, Mjawa na Bungu kwa ufadhili wa mradi wa Boost na Fedha kutoka Serikali Kuu.
Boost ni Mradi endelevu wa kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji kwa kuboresha miundombinu ya Elimu kwa shule za Awali na Msingi. Katika Wilaya ya Kibiti Mradi huu unatekelezwa katika maeneo ya Kata mbalimbali kama Bungu, Mjawa , Mlanzi, Mtawanya, na Ruaruke.
Wakiwa katika Kata ya Mtawanya Kitongoji cha Makima wamekagua eneo la ujenzi wa nyumba mbili kwa moja za walimu wenye thamani ya sh. 50,000,000 utakao tekelezwa kwa fedha za Serikali Kuu na katika shule hiyo hiyo kupitia mradi wa Boost jumla ya sh 73,000,000 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vipya 3 vya madarasa sambamba na ujenzi wa matundu 4 ya vyoo na ujenzi huo unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa mara tu fedha zitakapoingia.
Vilevile timu hiyo ambayo imeongozwa na Mlenduka imetembelea na kukagua maeneo ya ujenzi wa Shule mpya za Jaribu Magharibi na Bungu wenye thamani ya sh 306,900,000 kwa kila shule kwa ufadhili wa fedha za Boost.
Katika maeneo hayo yaliyokaguliwa kwa kila shule kutajengwa vyumba 7 vya madarasa, vyoo matundu 16, vyumba 2 vya madarasa ya awali ya mfano, Jengo la Utawala, kichomea taka, makabati na kifaa cha kuhisi moto (Smoke detector).
“Huu ni mradi mpya kabisa utakaokuwa wa mfano, tushirikiane kwa kila namna kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati na viwango vyenye ubora wa hali ya juu” alisema Mlenduka.
Hata hivyo mara baada ya ukaguzi wa kitaalam Kaimu Muhandisi wa Wilaya, Muhandisi Juma Kubadesha amethibitisha kuwa, maeneo yote aliyokagua yanafaa kwa ujenzi. Pia amewaagiza watendaji kuhakikisha wanafanya usafi kwenye maeneo hayo, tayari kwa maandilizi ya ujenzi utakaozingatia mpangilio mzuri wa majengo na kwa kufuata michoro ya ramani elekezi.
Aidha Watendaji hao wamesema Mradi wameupokea kwa furaha kubwa, na wananchi wapo tayari kujitolea kwa ajili ya kuongeza nguvu kazi, kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.