Idara ya elimu sekondari Wilaya ya Kibiti imeendelea na zoezi la ufuatiliaji juu ya ufundishaji wa walimu na ujifunzaji kwa wanafunzi katika shule za sekondari ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa moja ya mbinu zinazoaminika kuwa ni mwarobaini wa kuongeza ufaulu mashuleni ndani ya Wilaya.
Katika kupandisha ufaulu shuleni kaimu Afisa Elimu sekondari mwl. Shaban Mangosongo aliye ambatana na wasaidizi wake, amewahimiza waalimu kuhakikisha wanatumia muda wao kufundisha kwa moyo kuhakikisha watoto wanaelewa na wanafanya vizuri katika masomo yao pindi wafanyapo mitihani lengo likiwa ni kuhakikisha kibiti inapandisha ufaulu na kutokomeza ziro kwani ni jambo linalowezekana.
Hayo yamebainishwa katika ziara ya siku 2 iliyohusisha shule za Sekondari za Mjawa,Nyambili Nyambunda, Msafiri, Mtawanya, Ruaruke, Jaribu, Mchumkwi na Kikale ambapo Mwl Mangosongo amewahusia wanafunzi kusoma kwa bidii na kuwashirikisha Walimu wao pale wanapokwama, ili kuweza kufanya vizuri katika mitihani yao na kuweza kufikia malengo yao.
“Ili kufaulu lazima kila mwanamfunzi awe na bidii ya kusoma na kufurahia somo, wekeni ratiba, mjenge tabia ya kujisomea kila siku baada ya masomo ya darasani. Alisema Mwl. Mangosongo.
Hata hivyo kaimu Afisa Elimu huyo, amewataka wanafunzi wote kuhakikisha wanafanya mazoezi ya kutosha ili kujiimarisha katika masomo mbalimbali Pamoja na kujibu maswali vizuri kipindi cha mitihni.
“Mnapofanya vibaya mitihani yenu na kushindwa kufanya vizuri, tunaumia sana, hebu mkasome kwa bidi ili pia kama Wilaya tuondokane na aibu ya kufeli na kushika nafasi za ovyo”. Alisema Mangosongo.
Aidha katika vikao hivyo ambavyo wazazi walishirikishwa pia, kwa pamoja wamekubaliana kuchangia pesa ya chakula cha mchana cha watoto shuleni ili kuimarisha afya za wanafunzi na kuwaepusha kusoma wakiwa na njaa.
Naye kaimu katibu msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Ally Habib Masoud aliwakumbusha Walimu kwa kutoa ufafanuzi wa nidhamu kwa Utumishi wa Umma huku akiwasihi kufanya kazi kwa kufuata sheria,miongozo, kanuni na taratibu zake. Pia aliwasisitiza Walimu kuhakikisha wanaujua na kuuelewa vizuri mfuko wa fidia za wafanyakazi kazini (WCF) ili kuweza kupata stahiki zao kupitia mfuko huo wapatapo majanga kazini.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.