NI KUFUATIA MAFURIKO YATOKANAYO NA MAJI YALIYOFUNGULIWA KUTOKA BWAWA LA KUFUA UMEME LA MWALIMU NYERERE.
18.3.2024
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo akiwa ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama, amewaagiza wakazi wa Kitongoji cha Beta Kata ya Mtunda na vijiji vyote vilivyopitiwa na delta ya Rufiji kuhamia maeneo yaliyoinuka ili kuepuka uwezekano wa uwepo wa maafa ya Mafuriko yanayotokana na maji yaliyofunguliwa katika bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere.
"Kutokana na hali ya maji ilivyo, niwatake tu muanze kuhama kuelekea katika maeneo yenye miinuko ili kuepuka maafa, maji yanaweza kuongezeka zaidi ikawa shida kutoka na tunaelekea katika msimu wa masika" Alisema Kanali Kolombo.
Kanali Kolombo akizungumza na wakazi hao wenye kaya zaidi ya 3096 amewasisitiza kuhakikisha wanatekeleza zoezi la kuhama haraka iwezekanavyo na mpaka kufikia tarehe 25.3.2025 wawe wamekwisha kuhama katika maeneo hayo.
Vilevile Kanali Kolombo amewaagiza watendaji Kata wote kusimamia zoezi Hilo kwa vitendo, kwa kushiriki kikamilifu shughuli za uokoaji katika maeneo yao na kutoa taarifa zilizo sahihi, kusimamia uundwaji wa Kamati za maafa katika ngazi ya Kata, vijiji na Vitongoji kwa mujibu wa Sheria.
Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Mtunda Mhe. Omari Twanga baada ya kufika katika Vitongoji hivyo amewataka wananchi wake kuchukua tahadhali kulingana na uhalisia wa wingi wa maji ikiwa ni pamoja na kuhama katika maeneo hayo ili kunusuru uhai wao.
Naye Afisa Tarafa ya Kikale Ndg. Salim Malogwa amesema ngazi ya Wilaya wamekwisha weka utaratibu wa wakazi hao kupokelewa katika maeneo yaliyosalama na kuendelea na shughuli za kila siku mpaka maji hayo yatakapopungua.
Awali siku moja kabla timu ya Wataalam kutoka bwawa la Mwalimu Nyerere ambayo imeweka kambi katika Wilaya ya Kibiti na Rufiji kwa lengo la kutoa uelewa na kuchukua tahadhari baada ya kufunguliwa maji kutoka katika bwawa hilo, walifika katika maeneo ya Beta, Nganyanga na kilindini kutoa elimu kwa wananchi hao sambamba na kujionea hali halisi ilivyo.
"Tulitarajia bwawa litajaa kwa muda wa miaka 3 lakini limejaa ndani ya mwaka 1 na miezi 3 na mitambo haijakamilika kujengwa hivyo inatulazimu tupunguze maji kwa kuyafungulia kupitia milango tuliyoweka kwa tahadhari ili kulinda bwawa lisibomoke" Alisema Mhandisi Dismas Mbote.
Kauli hiyo imekuja baada kufunguliwa maji kutoka katika bwawa la Mwalimu Nyerere kuanzia machi 5 na zoezi linatarajiwa kumalizika Mei, 25 mwaka huu. Mpaka sasa kiasi cha maji kilichofunguliwa ni 3,120m3/s (sawa na lita 3,120,000 kwa sekunde).
"Tuliaza kujaza bwawa tarehe 22.12. 2022. Leo kina cha maji kimefikia mita 183.26 (kati ya 184.00) juu ya usawa wa bahari. Maji yanayoingia bwawani ni mita za ujazo 3,558.50m3/s (lita 3,558,000 kwa sekunde) na Maji tunayopunguza (spill) ni 3,120.34m3/s (lita 3,120,000 kwa sekunde). Mpaka bwawa linajaa ni mita za ujazo billioni 31.906 (lita trillioni 31). Uwezo wa mwisho wa bwawa kupokea maji ni mita za ujazo bilioni 32 (lita trilion 32) na sasa Bwawa limejaa kwa asilimia (97.33%)" Alisema Eng. Mbote.
Naye Kaimu Meneja Mazingira wa Tanesco Makao Makuu Ndg. Tluway Sappa amewasisitiza wananchi kuepuka kusubiri madhara yatokee ndiyo waanze kuhama hivyo ni vema kuchukua tahadhari mapema kuelekea nchi kavu kabla maji hayajaongezeka.
"Niwasihi tu muhame sasa, toeni vitu vya muhimu mapema ikiwa ni pamoja na kubeba vyakula, msisubiri maafa yatokee ndipo muanze kuhangaika” Alisema Sappa.
Akizungumza na wakazi wa Beta Afisa Mazingira kutoka bwawa la Mwalimu Nyerere, Ndg. Yusuph Kamote yeye amewataka wananchi hao kuwa waangalifu katika kipindi hiki kwani maji husafiri na viumbe mbalimbali kama vile mamba, viboko, nyoka wakubwa n.k hivyo ni vema kuthamini uhai wao kwa kuhama mapema kabla maafa hayajayokea.
Aidha wakazi ya Vitongoji hivyo wamesema wako tayari kutoka maeneo hayo ili kuweza kunusuru maisha yao huku wakikiri uwepo wa ongezeko la wingi wa maji tofauti na ilivyozoeleka. Mpaka sasa tayari kuna familia zimehama na nyingine zinaendelea kuhama taratibu.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.