24.07.2024
Kampuni ya Jenga Tanzania Agriculture imetoa msaada wa Vifaa kwaajili ya kusaidia shughuli za lishe wilayani Kibiti. Hii ni katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kupunguza ama kuondoa kabisa hali ya Udumavu nchini ambao unaosababishwa na lishe mbaya.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni Mizani 2 ya kupima uzito na urefu kwa watu wazima, Mizani 2 ya watoto, Mizani 2 ya kupimia maziwa au chakula, Karatasi nyeupe rimu 1, Jagi za umeme 2, Chupa za chai 2, Faili ngumu pamoja na vifaa vingine vya shajala.
Akipokea msaada huo Katibu Tawala Wilaya ya Kibiti Bi. Maria Katemana amesema anaishukuru sana Jenga Tanzania kwa ushirikiano wao mzuri wa kuhakikisha watu wanakula lishe kulingana na uzito unaotakiwa lakini pia kwa kujali Afya za watoto ambao wakiwa na hali nzuri ya lishe watakuja kuwa vijana wenye akili nzuri na kuijenga Tanzania yetu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hemed Magaro ameshukuru kwa msaada wa vifaa hivyo kwani vinaenda kusaidia utoaji wa huduma za lishe kwa watoto lakini hata kwa watu wazima.
“Kwa watoto vitatusaidia kuwapima uzito na kujua hali zao za lishe na kama watakuwa wameathirika kuweza kuwapa matibabu, Japo kitengo kinasimamiwa vizuri na Afisa lishe lakini kwa vifaa hivi vinaenda kumsaidia kufanya kazi yake vizuri na kwa ufanisi zaidi” Alisema Ndg. Magaro.
Magaro ameiomba Kampuni hiyo kuendelea kushirikiana zaidi kwani Halmashauri inayo mambo mengi ikiwemo mambo ya Afya lakini pia mambo ya Elimu kote huko kunahitaji ushirikiano ili kuijenga Tanzania.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.