25.03.2024
Diwani wa Kata ya kibiti Mhe. Hamidu Ungando amewasihi wanawake wajasiliamali kuwa na tabia ya kuchukua mkopo kwa malengo ya muda mrefu na yenye kuleta tija na si kwa ajili ya kutunzana sambamba na kurejesha ili wahitaji wengine nao wapate fursa ya kukopa.
Awali Serikali ilisimamisha mikopo hiyo baada ya kusuasua kwa marejesho katika vikundi mbalimbali vilivyokopa ambapo sasa itatolewa kwa utaratibu mzuri tofauti na ilivyokuwa imezoeleka.
"Tunashukuru Mama, Mhe. Dkt. SSH Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kurejesha mikopo tena ambayo sasa itamwezesha mtu mmoja mmoja kukopa na kulipa peke yake na siyo mpaka kuwa na vikundi" Alisema Ungando.
"Awamu hii mikopo mtakayopewa haitahususha fedha bali mtapewa mahitaji unayohitaji katika biashara uliyoainisha" Alisema Mhe Ungando.
Hayo yamejiri katika kikao cha mafunzo ya jukwaa la wanawake wajasiliamali Kata ya Kibiti kilichoandaliwa na kuratibiwa na Afisa Maendeleo ya jamii wa Kata hiyo Ndg Geoffrey Haule kwa lengo la kuwapatia elimu na kuwajengea uwezo wa kuweza kuendesha biashara na kupata mikopo inayorejesheka yenye masharti nafuu kwa kuainisha biashara na kujiunga katika vikundi.
Afisa Maendeleo huyo amesema Dhumuni kubwa la kuwezesha mafunzo hayo ni kutoa elimu juu ya ujasiliamali, utoaji wa mikopo, utunzaji wa kumbukumbu na faida, ukuzaji na upatikanaji wa masoko kupitia mitandao ya kijamii, kupinga ukatili wa kijinsia, ndoa, mimba za utotoni na utoro mashuleni. Dhumuni lingine ni kutoa elimu ya malezi ya familia, kufanya biashara wanazopenda kwa ubunifu zinazovutia wateja kwa urahisi.
Katika kufanikisha mafunzo hayo yenye mada mbalimbali Ndg. Haule ameshirikiana na wadau wengine wa maendeleo kutoka Wilaya ya Kibiti ambao ni Afisa Ustawi wa jamii, dawati la jinsia, Afisa biashara, Madiwani viti maalum, viongozi wa jukwaa la wanawake, viongozi wa vyama ngazi ya Kata na Wilaya, Katibu wa chama cha walimu na makundi maalum.
Wakitoa nasaha mbalimbali kwa nyakati tofauti viongozi waalikwa wakiongozwa na Madiwani wa viti maalum wamewataka wajasiliamali hao kuhakikisha waliyofundishwa wanayafanyia kazi kwa maendeleo yao binafsi na Kibiti kwa ujumla.
Mara baada ya mafunzo kukamilika wajasiliamali hao wameonekana kuelewa na kuhamasika, jukwaa hili limekuwa na mvuto wa kipekee kutokana na namna walivyojitokeza kwa wingi ambapo kulikuwa na jumla ya wanawake 260.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.