7.3.2024
Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imeadhimisha Juma la Elimu sambamba na utoaji wa TUZO kwa shule, wanafunzi na walimu waliofanya vizuri kitaaluma kwa Idara zote yaani elimu ya Msingi na Sekondari, bila kuwasahau wadau mbalimbali wa Elimu waliochangia ufaulu zikiwemo Taasisi pamoja na Wahe. Madiwani. Maadhimisho hayo hufanyika nchi nzima kila mwaka ifikapo mwezi wa tatu.
Katika hafla hiyo shule binafsi ya WAMA NA KAYAMA imeongoza kwa kwa kupata zawadi nyingi zilizotolewa kwa wanafunzi na walimu kwa ujumla katika michepuo mbalimbali ya masomo na ufaulu wakifuatiwa na shule ya Serikali ya Sekondari ya Wavulana Kibiti.
Lengo la maadhimisho ya sherehe hiyo ni kuongeza hamasa kwa wanafunzi na walimu kuendelea kupambania Sekta ya Elimu izidi kusonga mbele. Halmashauri ya wilaya ya Kibiti imetumia fursa hii kutoa zawadi kutokana na kuongezeka kwa hali ya ufaulu ndani ya Wilaya ukilinganisha na ilivyokuwa awali.
Zawadi zingine zimekwenda kwa wanafunzi waliopata Daraja la kwanza kutoka katika shule za Sekondari za Kata za Mtawanya na Mjawa ambapo upande wa Elimu ya Msingi shule zipatazo 10 kati ya 89 zimeongoza kwa kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kupewa zawadi pia.
Licha ya walimu na wanafunzi kupatiwa zawadi Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amepatiwa TUZO (ngao) ya usimamizi mzuri, jitihada, maarifa na maelekezo yake kuwa nguzo ya kupandisha ufaulu kwenye mitihani ya Taifa kwa elimu ya Msingi na Sekondari 2023.
Viongozi wengine waliopatiwa zawadi ni Diwani wa Kata ya Bungu Mhe. Ramadhan Mpendu, Diwani wa Kata ya Kibiti Mhe. Hamidu Ungando na Diwani wa Mtawanya Mhe. Malela Tokha.
Akisoma taarifa ya Idara ya elimu Afisa Elimu Sekondari Mwl. Anna shitindi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji amekiri kuongezeka kwa hali ya ufaulu ukilinganisha na ilivyokuwa awali.
"Ni kweli hali ya ufaulu imeongezeka, lakini walimu msibweteke tunataka tutoke hapo tulipo tupande zaidi, na inawezekana tukiongeza jitihada za ufundishaji na ushirikiano" Alisema Shitindi.
Vilevile Mwl Shitindi amesema, pamoja na changamoto zolizopo wamejiwekea mikakati ya kutafuta mwarobaini wa kuongeza ufaulu pamoja na kuhamasisha jamii kuchangia chakula shuleni, kuhamasisha jamii juu ya uanzishwaji wa Ujenzi wa miundombinu kulingana na vipaumbele, kuimarisha ushirikiano kati ya walimu na wazazi , kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia n.k.
Hata hivyo Mwl. Shitindi amesema ili Wilaya iweze kufikia malengo ya ufaulu vizuri wanahitaji kuungwa mkono katika masuala mbalimbali, kama vile kugharamia uchapishwaji wa mitihani ya kujipima shuleni, kuachana na tamaduni zilizopitwa na wakati, kutokomeza ukatili wa kijinsia, kujitolea katika miradi ya elimu na kuchangia chakula cha mchana shuleni.
Akimwakilisha Mgeni rasmi SP Matulanya, Paschal Kabogo Mkuu wa Gereza Wilaya ya Kibiti amewashukuru viongozi, walimu pamoja na wadau wa elimu kwa ushirikiano mzuri ambao jitihada zake zimeleta kuongezeka kwa ufaulu japokuwa bado wanahitaji kuongeza juhudi zaidi ili kufikia malengo ya ufaulu wa juu zaidi.
"Walimu bado mna kazi kubwa ya kuongeza bidii katika ufundishaji, suala la kuongezeka kwa ufaulu huu ndani ya Wilaya ni faraja kubwa kachapeni kazi mnaweza" Alisema SP Matulanya.
Aidha, SP Matulanya amempongeza Mkurugenzi Mtendaji Ndg Hemed Magaro kwa kutoa motisha (fedha taslimu na Vyeti) za kuwatunuku walimu wenye uzalendo na jitihada za kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinaongezeka katika Wilaya sambamba na zawadi za wanafunzi waliofanya vizuri na kufaulu katika masomo yao kwani unakwenda kuwa chachu kwa wengine ili nao wajitahidi kufanya vizuri.
Kipekee SP Matulanya amemshukuru Mhe. Rais Dkt. SSH ambaye kwa kiasi kikubwa katika Serikali yake amepambana kutatua changamoto nyingi za elimu hususani katika miundombinu ya shule na fedha za uendeshaji wa shule kupitia mfumo wa elimu bila malipo.
Naye Katibu wa Chama cha Cha Mapinduzi ndg Zacharia Muhidini, Makamu Mwenyekiti wa baraza la Wahe. Madiwani wa Halmashauri Mhe. Omary Twanga wamesema kwa ujumla wanatambua umuhimu wa walimu kutokana na kazi kubwa wanazofanya kuhakikisha Taifa linakuwa na wasomi kwa kuwafundisha na kuwalea vema shuleni.
"Walimu mchango wenu tunautambua, changamoto zenu tunazijua, tuwaombe tu msikate tamaa, maombi yenu, kero tumepokea tutayafanyia kazi na mengine tunaendelea kutekeleza kadri fedha zitakavyopatikana." walisema.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.