Kamati hiyo ilipita na kukagua miradi ifuatayo:
1.Ujenzi wa nyumba za Walimu 2 kwenye jengo moja (2 in 1) katika shule ya Msingi kikale inayojengwa kwa kutumia MAPATO YA NDANI mpaka sasa Halmashauri imepeleka Tsh. 18,600,000.00, ujenzi umefikia hatua ya kupaua.
2.Ujenzi wa matundu ya Vyoo, Kinawia mikono, Mnara wa maji na Kichomea taka katika Zahanati ya Rungungu, mradi umekamilika kwa kutumia Tsh. 37,700,000.00 ambazo ni fedha za SANITATION.
3.Kiwanda cha Ukamuaji wa mafuta ya mawese kinachoendeshwa na Kikundi cha Vijana Uchumi Ruaruke A ambacho kimewezeshwa kwa kupewa Mkopo wa Tsh. 20,000,000.00 na Halmashauri kutoka kwenye MAPATO YA NDANI, Kiwanda kimekamilika lakini kinafanya kazi kwa kusuasua.
4.Mashine ya Kusaga na kukoboa nafaka inayoendeshwa na kikundi cha Tushikamane Nyamatanga. Kikundi kimewezeshwa kwa kupewa Mkopo wa Tsh. 10,000,000.00 na Halmashauri kupitia MAPATO YA NDANI. Mashine imekamilika na inafanya kazi vizuri.
5.Ujenzi wa shule ya sekondari ya Wananchi katika Kata ya Kibiti, mpaka sasa imetumia Tsh. 38,000,000.00 ambayo ni nguvu ya wananchi kujenga maboma ya madarasa 4 na katika kuunga mkono juhudi hizo za wananchi kwenye ukamilishaji MFUKO WA JIMBO umetoa Tsh. 5,400,000.00 na Halmashauri imepeleka Tsh. 10,000,000.00 kutoka kwenye MAPATO YA NDANI, Ujenzi upo kwenye hatua ya umaliziaji wa maboma ili kupaua.
6.Biashara ya huduma za kifedha na gesi inayoendeshwa na Bi. Zainabu Kwangaya ambaye aliwezeshwa kwa kupewa mkopo wa Tsh. 7,000,000.00 kutoka kwenye MAPATO YA NDANI. Biashara hii inaendelea vizuri.
Baada ya kuiona miradi yote wajumbe walitoa mapendekezo yao kwenye majenzi yote yaliyokamilika na yanayoendelea kwa kumtaka Mhandisi kufanya marekebisho haraka kabla ya kuendelea na shughuli zingine ambapo hitilafu ndogondogo kwenye kuta ndiyo tatizo lililoonekana Zaidi.
Kwa kikundi cha Vijana Uchumi Ruaruke A, kamati ilisimama kidete kuwa ni lazima kikundi hicho kirejeshe fedha hizo kwakuwa walichopewa kilikuwa ni mkopo na sio msaada.
“Vijana wetu tumewasikia, pamoja na changamoto mlizokutana nazo kwenye biashara yenu lakini bado ni lazima mzilipe fedha hizo. Mlichopewa kilikuwa ni mkopo na sio msaada, hizo ni fedha za Wananchi wa Kibiti hivyo ni lazima zirejeshwe ili na wengine wanufaike nazo” Alisema Mh. Omari Twanga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo.
Kwa Kikundi cha Tushikamane, Kamati ilisema imesikia maombi yao hivyo, wameyachukua na wanakwenda kujadili kwenye vikao vyao wanaamini maombi yao yatafanikiwa kwakuwa wameonesha nia ya dhati ya kurejesha mkopo wao.
Kikundi cha Tushikamane kiliomba kuongezewa muda wa marejesho kwakuwa walishindwa kufanya kazi kwa muda lakini sasa wanaendelea vizuri na wamekwisharejesha sehemu ya mkopo huo.
Aidha Kamati imemshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan kuendelea kuunga mkono juhudi za wananchi kwa kuwaletea Tsh. 350,000,000.00 ili kukamilisha maboma yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi na kuongeza majengo mengine ili shule hiyo ikamilike.
Kamati ilihitimisha ziara yake katika duka la Bi. Zainabu Kwangaya ambaye anaendelea vyema kutoa huduma za kifedha na uuzaji wa vifaa vya simu na gesi. Kila mmoja alimsifu mama huyo kwa ujasiri alionao kwakuwa licha ya ulemavu wa viungo alionao bado anaendelea kuipambania familia yake kwa kuendesha biashara yake na kufanya marejesaho vizuri, hivyo wanategemea akimaliza mkopo huo atachukua mwingine mkubwa zaidi ili aendelee kupanua biashara yake.
Kwa upande wake Bi. Zainabu amesema anamshukuru sana Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Mbunge wa Kibiti, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti pamoja na Diwani wake wa Kata ya Kibiti kwa jitihada zao za kuhakikisha makundi maalum yanainuka na kujitegemea kiuchumi. Mikopo wanayopewa imewasaidia sana kujitegemea.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.