Kuhakikisha Miradi inaendana na thamani ya fedha kwa kuzingatia viwango.
Waakuu wa idara na wasimamizi wa Miradi mbalimbali katika sekta za Umma Wilaya ya Kibiti, wametakiwa kuongeza umakini katika utekelezaji na ufuatiliaji wa Miradi inayotekelezwa kwa kuwajibika ipasavyo ili iweze kuleta tija kwa maendeleo ya Kibiti.
“Mkawajibike kutimiza majukumu yenu kama kanuni zinavyoelekeza, mliopo hapa mmeaminiwa kusimamia idara mlizopo, kila mmoja akajitume kuitendea haki nafasi aliyoaminiwa kuitumikia” Alisema Mhe. Ndaruke.
Hayo yamejiri katika ziara ya kamati ya Siasa Wilaya ilipotembelea na kukagua baadhi ya Miradi ya maendeleoinayotekelezwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 kwa lengo la kujionea hali halisi, Pamoja na kuongeza ufanisi.
Hata hivyo kamati imeiagiza idara ya manunuzi kununua vifaa kwa wakati ili kazi ya ujenzi iendane na muda uliokusudiwa kukamilisha Miradi husika.
Vilevile kamati ya Siasa imewataka Wataalam,wasimamizi,na Wakuu wa Idara, kujiridhisha katika kila hatua ya Mradi mapema kabla ya kwenda hatua nyingine ili kuepuka gharama za marekebisho ya makosa madogo madogo ya kiufundi hatimaye fedha zilizopangwa ziweze kukamilisha Miradi .
“Kabla ya kupiga hatua nyingine katika Miradi Wataalam piteni kujiridhisha, ndipo hatua nyingine ianze ili kuepuka kupata hasara ya kuongezeka kwa gharama”Alisema Mwenyekiti Ndaruke.
Mbali na hayo kamati imesisitiza jitihada zifanyike kwa taasisi zinazotoa huduma kwa jamii ili kuimarisha Miundombinu ya Maji, Barabara na Umeme kwani bado ni changamoto katika maeneo mengi ya miradi jambo linalosababisha kuchelewesha maendeleo .
Pia Kamati hiyo imewaasa Watumishi wa umma na taasisi zote kutumia lugha nzuri katika maeneo ya kazi, kuwajali wananchi wanaowatumikia, kujituma ipasavyo ikiwa ni pamoja na kutekeleza mikakati iliyopangwa kwenye miradi inayoendelea na inayotarajiwa kuanza.
Kamati hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Bw. Juma Ndaruke ambayo iliambatana na viongozi mbalimbali wa Wilaya ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Idara na vitengo, wakuu wa Taasisi za Umma ilinzia katika kituo cha Nyamatanga kata ya Ruaruke ambapo walikagua ukarabati wa jengo la OPD, ujenzi wa maabara, Jengo la upasuaji, Jengo la kujifungulia, na Jengo la kuhifadhia maiti ambapo jumla ya sh 446,006,356.28 fedha za Serikali Kuu kupitia TASAF zimepangwa kutumika.
Ziara ikaendelea katika Hospitali ya wilaya ambapo walikagua uendelezaji wa ujenzi wa jengo la upasuaji, wodi ya upasuaji kwa wanawake na wanaume pamoja na Jengo la kuhifadhia maiti ambapo jumla ya sh 800,000,000 fedha kutoka serikali kuu zinatumika Pia walikagua ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura lenye thamani ya sh 300,000,000 fedha za Uviko, kutoka Serikali Kuu.
Katika ziara hiyo pia walifika katika Kata ya Bungu kwenye mradi wa shule ya sekondari ya Nyambili Nyambunda yenye ujenzi wa vyumba 5 vya madarasa na ofisi ya walimu wenye jumla ya sh 100,000,000, kwa fedha za serikali kuu,ambapo ujenzi umekamilika na madarasa yameanza kutumika.
Mbali na miradi hiyo pia walitembelea Kata ya Mjawa kukagua ujenzi wa shule ya sekondari ya jaribu mpakani -SEQUIP iliyojengwa kwa fedha za serikali kuu (tozo za miamala ya simu) zenye jumla ya sh 470,000,000 na mapato ya ndani sh 30,231,000. na Kisha kukamilisha ukaguzi huo katika kituo cha afya Mjawa ambacho kinaendelea na ukamilishaji wa baadhi ya majengo huku kikiwa kinaendelea kutoa huduma za kitabibu.
Akiishuru kamati ya siasa, Mkuu wa Wilaya ya kibiti Kanali Joseph Kolombo amesema ziara na kikao kilichofanyika ni faida kwa Wataalam kwani kinawakumbusha Wakuu wa Idara kutekeleza ilani ya chama Tawala na kufuata miongozo ya kazi.
Nae kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mwl. Zakayo Mlenduka amesema kupitia ziara hiyo maagizo na changamoto zote zilizotolewa amezipokea na kuahidi kuzifanyia kazi kadri itakavyowezekana ili kuhakikisha malengo yanatimia.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.