12.08.2024
Kamati ya Siasa Wilaya ya Kibiti ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Juma K. Ndaruke imefanya ziara ya kutembelea na kukagua baadhi ya miradi ya maendeleo iliyotekelezwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Jumla ya Miradi 6 yenye thamani ya shilingi 631,802,640.00 imekaguliwa. Miradi hiyo ni Ujenzi wa chumba 1 cha darasa Shule ya Sekondari Dimani, Ujenzi wa Bweni la watoto wenye mahitaji maalumu Shule ya Msingi Kitundu, Ujenzi wa Shule na Umaliziaji wa vyumba 4 vya madarasa Shule Tarajiwa ya Sekondari ya Wananchi Kibiti, Ujenzi wa vyumba 3 vya madarasa na matundu 5 ya vyoo Shule ya Msingi Msafiri, Ujenzi wa vyumba 3 vya madarasa Shule ya Msingi Kinyamale na Umaliziaji wa vyumba 2 vya madarasa Shule ya Sekondari Jaribu.
Mhe. Ndaruke amesema ziara hiyo ni ya kawaida na lengo lake siyo kutafutana nongwa bali ni kuona kazi zinazotekelezwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi zimesimamiwa ipasavyo ili kuleta tija, pa kukosolewa pakosolewe na pa kupongezwa papongezwe.
Wakiwa kwenye ziara hiyo, Wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Kibiti wamepongeza sana Uongozi wa Halmashauri (Mhe. Mkuu wa Wilaya, Wahe. Madiwani, Katibu Tawala, Mkurugenzi Mtendaji pamoja na Wataalamu wote) kwa kazi nzuri ya usimamizi wa miradi hiyo kwani kote walikotembelea majengo yapo vizuri.
Aidha Kamati imesisitiza Samani zinazonuliwa kwaajili ya miradi hiyo ziendane na ubora wa majengo yaliyopo ili hadhi na thamani ya fedha zilizotumika ionekane.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Ndg. Hemed Magaro ameishukuru kamati kwa pongezi walizotoa baada ya kuona jitihada za Wataalamu kwenye usimamizi wa miradi hiyo, naye akitoa pongezi kwa Kamati hiyo kwani nao wanapambana sana ili Halmashauri ipate fedha za miradi huku akiahidi kufanyia marekebisho changamoto ndogondogo zilizoonekana.
Akihitimisha ziara hiyo Mh. Ndaruke amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha kwaajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo Kibiti, Uongozi wa Mkoa, Wilaya pamoja na Wananchi wa Kibiti kwa kusimamia vyema miradi hiyo.
“Niwashukuru sana wote mliohusika kwenye usimamizi wa miradi hii kwani mmesimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya Chama, hivyo sisi Wanasiasa tuna maneno mengi ya kusema huko kwenye majukwaa kwa kazi hii kubwa mliyoifanya”
“Lakini pamoja na pongezi hizi nyingi mlizopata msiende kubweteka, ukisifiwa maana yake mazuri ni mengi kuliko mabaya kwahiyo mkaendeleze haya mazuri mliyioanzisha” Alisema Ndaruke.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.