KANALI KOLOMBO AAHIDI KUMALIZA MGOGORO WA ARDHI (MIPAKA) MTAWANYA.
20.6.2023.
MKUU wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amekutana na wanachi wa Kata ya Mtawanya kutafuta muafaka wa mgogoro wa mipaka kati ya wananchi na Uongozi wa shule ya sekondari ya wavulana Kibiti, ambao umekuwa ni changamoto ya muda mrefu katika Kitongoji cha Magogo matatu.
Katika mkutano huo uliofanyika Sekondari ya Mtawanya Kanali Kolombo amewataka wananchi hao kuwa wavumilivu na watulivu wakati muafaka unatafutwa kwa kufuata taratibu stahiki ili kuweze kupata suluhisho.
"Kuweni wavumilivu, hakuna mtu wa kuwahamisha kabla ya kupata suluhisho, eleweni kwamba ninyi nyote ni watoto wa baba mmoja na baba yenu ni Serikali hivyo hana budi kuwasikiliza watoto wake. "Alisema Kolombo.
Akiwa katika mkutano huo Kanali Kolombo amesema, ili kupata muafaka lazima kuwepo kwa maelewano ya pande zote mbili kwa maridhiano ya kupima mipaka upya, na kujua ukubwa wa eneo la shule.
"Ninawaahidi baada ya kupimwa na kujua idadi ya wanakaya, nitakwenda kulijadili na ngazi ya mkoa tuweze kupata maamuzi ya haraka kabla ya 2025" Alisema Kanali Kolombo.
Hata hivyo Diwani wa Kata ya Mtawanya Mhe. Malela Salum Tokha, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kulipa kipaumbele swala hilo na kumweleza kwamba mgogoro huo usipomalizika mapema utaleta changamoto kwa shughuli za kimaendeleo hususani katika kilimo ambapo Kata hiyo ni miongoni mwa Kata zinazofanya vizuri kiuzalishaji na endapo wakiendelea kukosa maelewano hali itakuwa tofauti.
"Mtawanya hatuna tatizo, jambo zito linalotusumbua Kata hii ni mgogoro wa muda mrefu, wa wananchi na shule, tunaomba mtutatulie." Alisema Mhe. Diwani Tokha.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kitongoji cha Magogo matatu Mwenyekiti wa Kamati ya kufuatilia mgogoro huo ndg Rashid Musa Mkinga amesema ikumbukwe kwamba kabla ya ujenzi wa sekondari palikuwa na wananchi ambao ni wazawa wa Magogo matatu, hivyo walirudi kwenye maeneo yao baada ya kuruhusiwa kurudi maeneo yao ya asili katika miaka ya 1990 na kuelekezwa kuweka makazi ya kudumu.
Hata hivyo Mkinga alidai kuwa kiini cha mgogoro ni madai ya Kibiti sekondari kuwa eneo la Magogo matatu lenye hekari 4000 ni mali ya shule wakati huo huo wananchi nao wakidai ni eneo lao la asili toka enzi hizo, ambapo wao ndiyo walioruhusu shule kujengwa eneo hilo.
Akifunga mkutano Mwenyekiti wa Kijiji cha Magogo matatu amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuitikia wito huku akisema ujio wake umewaondoa hofu wananchi wake na ni matumaini yake kwa niaba ya wananchi mgogoro utakwisha salama.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.