Mkuu wa wilaya ya Kibiti kanali Joseph Kolombo ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kuwakumbuka watoa huduma wa vijiji (Wavi) ambao husaidia kutoa huduma, kufuatilia na kuripoti taarifa za hali ya lishe ya vijiji.
Hayo yamejiri leo Julai 11, 2024 katika kikao cha tathmini ya Mkataba wa lishe ngazi ya Kata kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo moja ya changamoto iliyowasilishwa na Afisa lishe Wilaya ni ucheleweshwaji wa taarifa kutoka kwa watendaji kata ambao nao walisema wanapata changamoto kupata taarifa hizo kutoka kwa WAVI kwani wanaonekana kutojali uharaka wa taarifa hizo kwakuwa imekuwa ni kazi ya kujitolea zaidi kwao bila malipo.
“Mkurugenzi naomba ulichukue hili, muwafikirie hawa WAVI kwakuwa ni watu muhimu sana ambao wanatusaidia kule vijijini” Alisema Kanali Kolombo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Bw. Denis Kitali amesema kwakuwa jambo hilo limekaa kibajeti zaidi Halmashauri imelichukua na litashughulikiwa kwahiyo WAVI wawe na subira na waendelee kutoa huduma.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa robo tatu, Afisa lishe Wilaya Bi. Roina Daza amesema kitengo cha lishe wilaya kimefanikiwa kufanya shughuli zifuatazo: Kutembelea na kutoa Elimu ya lishe kwenye Vijiji, Shule za Msingi na Sekondari pamoja na gereza la Mng’aru. Kufanya usimamizi shirikishi katika vituo vya kutolea huduma za Afya na kutembelea na kutoa matibabu kwenye familia zenye watoto wenye hali mbaya ya lishe.
Aidha Bi. Roina pia amesema hali ya lishe kwenye kata zote imeendelea kuimarika, 98.9% ya vijiji vimefanikiwa kufanya siku ya lishe ya Kijiji (SALIKI), 97.98% ya shule zinatekeleza mpango wa chakula mashuleni, idadi ya watoto wenye utapiamlo mkali imepungua huku kukiwa hakuna kifo cha mjamzito kilichotokea kwa robo husika.
Akifunga kikao hicho Kanali Kolombo amewataka Watendaji wote kwenda kutekeleza na kusimamia yote waliyokubaliana ikiwemo kutoa taarifa za hali ya lishe ya Kata zao kwa wakati ili kusaidia kufanikisha lengo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kuwa huduma za lishe zinaendelea vizuri katika maeneo yetu.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.