MKUU wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amefanya ziara ya kujiridhisha na kujionea maeneo ambako shule mpya za mfano zitajengwa katika Kata za Mjawa eneo la Jaribu Magharibi na Kata ya Bungu baada ya mapokezi ya kiasi cha Tsh. 821,000,000/= kwa ufadhili wa mradi wa Boost kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo.
Boost ni mradi endelelevu wa kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji kwa kuboresha miundombinu ya elimu kwa shule za awali na msingi. Katika Wilaya ya Kibiti mradi huu unaotekelezwa katika maeneo ya Kata mbalimbali kama Bungu, Mtawanya, Mlanzi, Mjawa na Ruaruke.
"Nimekuja hapa kujiridhisha kuona maeneo kutakapojengwa shule mpya, nimeridhika kabisa na eneo linafaa kwa ujenzi wa shule" Alisema Kanali Kolombo.
Akikagua maeneo hayo kwa nyakati tofauti, Kanali Kolombo amewataka wananchi waliojitokeza kusafisha eneo la ujenzi, kuupokea mradi huo na kusimamia vizuri ili uweze kukamilika kwa wakati huku akiwataka wananchi hao kuendelea kujitolea ili kuongeza nguvu kazi katika ujenzi Kwa maendeleo ya watoto wao.
" Nawapongeza kwa namna mlivyojitoa leo kusafisha eneo hili la ujenzi, endeleeni kujitoa katika shughuli hizi za kijamii kwa ajili ya maendeleo yenu" .Alisema Kanali Kolombo.
Aidha Afisa mazingira wa Wilaya Zakayo Gideon mara baada ya kukagua eneo hilo amewapongeza wanavijiji hao kwa kuchagua meneo mazuri kwani yanafaa kwa ujenzi huo kutokana na Mazingira ya eneo husika.
Hata hivyo katika maeneo yaliyokaguliwa katika kila shule, kutajengwa vyumba 7 vya madarasa ya shule za msingi, vyumba 2 vya madarasa ya awali, matundu 10 ya vyoo, Jengo la Utawala, kichomea taka, matundu 6 ya vyoo na kihisia moto kwa ufadhili wa mradi wa Boost.
Katika ziara hiyo Kanali Kolombo aliambatana na baadhi ya kamati ya ulinzi na usalama, Mkurugenzi Mtendaji, Afisa Elimu divisheni ya awali na msingi, Mhandisi wa Wilaya, Afisa ardhi, Afisa Mazingira, Afisa Maendeleo ya Jamii na Afisa mipango.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.