Hatimaye mwaronaini wa mgogoro wa ardhi kati ya shule ya sekondari ya wavulana Kibiti na wa magogo matatu katika Kata ya Mtawanya umepatikana baada ya pande zote mbili kuridhiana kwa kutumia mipaka ilivyotumika mwaka 2012 kupanga maeneo hayo.
Akisoma makubaliano yaliyofikiwa katika mgogoro huo, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amesema, muafaka umepatikana kwa kufuata maelekezo ya mpango wa Serikali ambao umesimamia maslahi ya pande zote mbili.
Kanali Kolombo amesema kwa mujibu wa maelekezo ya mpango huo, mipaka iliyowekwa mwaka 2012 ifuatwe na kuimarishwa na wananchi wa magogo matatu wataendelea kuishi katika maeneo yao na kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
"Leo tumemaliza mgogoro huu, ni wakati wenu sasa kufanya maendeleo hapa na kutenga maeneo ya huduma za kijamii, kama shule na zahanati" Alisema Kolombo.
Vilevile Kanali Kolombo ameziagiza Taasisi za maji na umeme Wilaya ya Kibiti, kufanya upembuzi yakinifu na kuhakikisha wanawafikishia huduma hizo wananchi wa magogo matatu.
Hata hivyo Diwani wa Kata ya Mtawanya Mhe. Malela Tokha, amempongeza Kanali Kolombo kwa kumaliza mgogoro huo kwa muda mfupi huku akimwomba Mkuu huyo wa Wilaya kusaidia zoezi la uwekaji wa mawe ya msingi na mipaka kufanyika kwa haraka ili kuepuka matatizo kujirudia.
"Mhe. Mkuu wa Wilaya kwa niaba ya wananchi tunakupongeza sana ila tunaomba utusaidie zoezi la uwekaji mawe ya msingi na mipaka lifanyike kwa haraka, tuwe huru kufanya maendeleo yetu" Alisema Mhe. Malela.
Aidha Mwenyekiti wa Kamati ya ufuatiliaji Mzee Rashid Musa Mkinga amesema mbali na mgogoro huo kuisha kwa amani, ameomba Kijiji cha Magogo matatu kipewe maandishi na nakala ya Ramani kama sehemu ya uthibitisho wa kuishi maeneo hayo kihalali.
" tunaomba tupewe barua yenye maandishi ya kumalizika kwa mgogoro huu na nakala ya Ramani ambayo inathibitisha uhalali wa kuwepo eneo hili, ikawe sehemu yetu ya ushahidi endapo itatokea sintofahamu" Alisema Rashid Mkinga.
Mwisho Mzee Rashid Mkinga amewataka wananchi wa Kitongoji cha magogo matatu kuchangamkia fursa kwa kutenga maeneo ya miundombinu ya kijamii kama vile kutenga maeneo ya shule na zahanati kwa maendeleo yao wenyewe n.k.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.