Mkuu wa wilaya ya kibiti Kanali Joseph Kolombo amewaagiza watendaji wa vijiji, Mtendaji wa Kata ya Mjawa na Afisa kilimo wa wilaya kupata takwimu za wakulima na wafugaji wote ikiwa ni pamoja na idadi ya mifugo ili kuweza kurahisisha zoezi la kutenga maeneo ya ufugaji na kilimo sambamba na kutambua maeneo yaliyo wazi.
“Nahitaji kupata takwimu ya wakulima ,wafugaji na idadi ya mifugo ili tuweze kuwatengea maeneo ya kudumu, Mtendaji Kata na Afisa kilimo nendeni kwa wafugaji mkapate takwimu sahihi za mifugo na wafugaji ili tujue namna ya kuwatafutia maeneo ya kuchungia” Alisema Kolombo.
Hayo yamejiri katika kikao cha wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Uchembe Kata ya Mjawa ambapo wakulima wamewalalamikia wafugaji kulisha mifugo katika mashamba na wakati huo huo wafugaji pia wamedai kukosa maeneo ya malisho kwasababu wakulima wamelima mpaka kwenye maeneo ya kuchungia jambo linalosababisha wao kuhangaika kutafuta maeneo ya malisho.
“Ni kweli tunapita kutafuta maeneo ya malisho kwani wamelima mpaka maeneo tunayolishia mifugo yamebaki maboma tu.”alilalamika mwakilishi wa wafugaji Bw. Ninini Mgusa.
Akiwa kijijini hapo Mkuu wa Wilaya Kanali Kolombo ametoa maelekezo kwamba kila mkulima alime eneo lililotengwa kwa kilimo na mfugaji achunge katika eneo lililotengwa kwa ajili ya ufugaji vinginevyo ni kukiuka kanuni taratibu na Sheria zilizopo.
“wakulima ,wafugaji nyie wote ni watu wangu,sipendezwi hata kidogo na malumbano yanayotokea, muheshimiane na kupendana” Alisema Kolombo.
Mbali na kero hizo amewataka wakulima kulima kwa wingi ili wapate mazao ya kutosha sambamba na kutoa taarifa endapo kutatokea tatizo na kuwataka wafugaji waendelee kufuga katika maeneo waliopangiwa kulisha wakati serikali inatafuta maeneo maalum kwa ajili ya malisho. Pia ameagiza kukamatwa kwa mkulima au mfugaji yeyote atakayekiuka sheria zilizowekwa.
“tutawaondoa wafugaji hapa baada ya kupata takwimu na maeneo maalumu ya kulishia mifugo yao na baada ya hapo kwa yeyote atakaye kiuka makubaliano haya tutamwajibisha ipasavyo” Alisema Kolombo.
Vilevile amewataka wakulima kutumia msimu huu wa mvua vizuri kwa kuhakikisha wanalima mazao ya kutosha ili kuweza kuvuna kwa wingi.
Aidha Kanali Kolombo ametembelea na kukagua shule ya sekondari Jaribu mpakani, kituo cha Afya Mjawa na Hospitali ya wilaya na kwa nyakati tofauti amesisitiza kuhakikisha miundombinu muhimu (maji,umeme na vyoo) inapatikana kwa haraka ili kuweza kurahisisha utoaji wa huduma kwa ufasaha .
Naye Afisa kilimo, mifugo, uvuvi na ushirika Ismail Bainga amewasihi wakulima katika kipindi hiki kuhakikisha wanatumia dawa/viwatiifu kuangamiza wadudu wanaoshambulia mpunga na mazao mengine .
Naye mkuu wa polisi wilaya ya kibiti (OCD) amewasihi wananchi wa Uchembe kutoa ushirikiano wa kiusalama katika maeneo yao, kutii sheria bila shuruti, kutoa taarifa Kwa wakati na usahihi na kuepuka kujichukulia sheria mkononi huku akikemea suala la ndoa katika umri mdogo na mimba za utotoni.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.