12.09.2024.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndg. Hanan Bafagih na Wataalam wake kuangalia namna ya kuhakikisha mifumo inafanya kazi kwa wakati ili kuepuka kuchelewa kuanza kwa miradi mara tu baada ya fedha kuingia kwenye akaunti.
"Hii Mimi sipendi, fedha za Ujenzi huu zimeingia tangu tarehe 23.06.2024 mpaka sasa zimekaa tu kwenye akaunti Ujenzi haujaanza haipendezi hata kidogo" Alisema Kolombo.
Kanali Kolombo amesema hayo alipokuwa akizindua Ujenzi wa shule Shikizi mpya ya Sekondari katika Kata ya Bungu wenye thamani ya sh 528,998,424 ambazo ni fedha za SEQUIP. Mradi huo unatarajiwa kuanza kutelelezwa wakati wowote kuanzia sasa.
Mkutano huo ulifanyika Bungu katika soko la TASAF ambapo Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza viongozi hao kuhakikisha maeneo yote yenye miradi yanapimwa na kupewa hati hii ni pamoja na miradi ya BOOST , VETA, SEQUIP n.k.
Kwa nyakati tofauti akifungua na kufunga mkutano huo Diwani wa Kata ya Bungu na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Ramadhan Mpendu amemshukuru Mhe. Rais Dkt. SSH na wasaidizi wake kwa miradi inayoendelea kuletwa Kibiti.
Awali akisoma taarifa fupi ya utekelezaji wa Ujenzi wa shule hiyo mpya Mkuu wa shule ya Sekondari Msafiri Mwl. Estomic Kimwemwe amesema Ujenzi utahusisha vyumba vya madarasa, Ofisi moja ya walimu, jengo la Utawala, Maabara za kemia, baolojia ,fizikia , maktaba, jengo la tehama, vyoo matundu 4 ya Wavulana na 4 ya Wasichana, kichomea taka na tanki la maji la ardhini.
Hata hivyo Mwl. Kimwemwe alifafanua kuwa Ujenzi utahusisha wazabuni tofauti tofauti kwa idadi ya majengo na mgawanyo wa matumizi kama ambavyo mchanganuo unavyoonekana katika chati.
Aidha Wananchi wa Bungu kipekee nao wamemshuru Mhe. Rais kwa kuendelea kutoa fedha za miradi katika Wilaya ya Kibiti huku wakikiri kuwa mradi wameupokea na wako tayari kutoa ushirikiano kuhakikisha Ujenzi unakamilika na kwa kuanza tu wamekwishaanza kusafisha eneo ambalo Ujenzi utatekelezwa.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.