16.01.2024.
Mkuu wa wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amefanya mkutano na wafanyabiashara katika soko la Kibiti ili kusikiliza na kutatua changamoto wanazokutana nazo.
Baadhi ya changamoto walizowasilisha wafanyabiashara hao ni uwepo wa bei isiyorafiki ya kukodisha vizimba vya biashara katika soko la Kibiti hivyo wameomba kupunguziwa kodi hiyo kutoka Tsh. 8,000 hadi Tsh. 7,000/= kwa mwezi kutokana na ugumu wa maisha uliopo, Pili kupunguziwa kodi kwenye baadhi ya mazao kama mpunga, Tatu kufanyiwa marekebisho katika choo cha zamani kilichokuwepo kwenye soko hilo ili kiweze kutumika tena pamoja na kuongezewa jengo la soko kwakuwa sasa kuna wafanyabiashara wamekosa maeneo hivyo wanafanya biashara zao maeneo ya wazi ambapo hukumbwa na adha ya hali ya hewa kama vile jua, mvua na hata upepo.
Akijibu changamoto hizo Kanali Kolombo aliwaambia mambo yote waliyomueleza ameyachukua, anakwenda kuyafanyia kazi. Kuhusu soko jipya, amewataka wafanyabiashara hao kuhakikisha wanajaza kwanza soko lilopo kwakuwa wengi wamehama sokoni na kufanya biashara nje. Kamati ya uongozi wa soko hilo imetakiwa kufanya mapitio ya wafanyabiashara waliopo pamoja na vizimba vilivyopo ili kujua upungufu uliopo ikiwa soko hilo litajaa. Lakini pia alimuagiza Mhandisi wa wilaya kuhakikisha choo wanachohitaji, kikarabatiwe na kianze kazi ndani ya siku saba.
Aidha Kanali Kolombo ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wananchi wote wenye watoto wanaopaswa kuanza shule kwa elimu ya awali na darasa la kwanza wahakikishe wanawaandikisha watoto hao na wale wenye watoto waliofaulu kwenda kidato cha kwanza wanakwenda kuripoti katika shule walizopangiwa ndani ya wiki hii hata kama hawana sare za shule.
“Nawaomba wananchi msiutafute mkono wa Serikali kwa nguvu. Watoto wote waliofaulu waende shule. Nimewaomba Polisi waongeze ukubwa wa mahabusu ili iwatoshe wazazi wote watakaokaidi agizo hili na sitasita kuwapeleka ndani” Alisema Kanali Kolombo.
Pia Kanali Kolombo amewaomba wananchi kuchangia chakula ili watoto waweze kula shuleni kwakuwa wanateseka sana kukaa na njaa muda mrefu, sambamba na hilo ameagiza kila shule iwe na bustani ya mihogo na mahindi ili kijihakikishia uwepo wa chakula muda wote.
Akihitimisha mkutano huo amewataka wazazi wote wenye watoto waliopata mimba shuleni kuhakikisha watoto hao wanarudi shule punde baada ya kujifungua na kuwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari juu ya magonjwa ya mlipuko kwa kudumisha usafi.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.