Wakati Tanzania ikiungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha siku ya mzingira leo 5/6/2023 Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imeadhimisha siku hii katika Kijiji cha Nyamisati Kata ya Salale wakati kimataifa hufanyika nchini Ivory Coast.
Maadhimisho hayo yenye Kauli Mbiu isemayo "Pinga uchafuzi wa mazingira, unaotokana na taka za plastiki", Kitaifa yamefanyika katika Jiji la Dodoma kwa kufanya usafi wa Mazingira katika eneo la barabara ya Jakaya Kikwete, kuelekea Jengo la Chamwino na Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdori Mpango.
Siku hii iliamuliwa na kupitishwa mwaka 1972 nchini Sweeden katika mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa, uliohusu masuala ya mazingira, ambapo lengo kuu lilikuwa ni kuelimisha wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi na usimamizi wa mazingira, ili waweze kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira duniani.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mgeni rasmi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Salale, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira Wilayani Kibiti Mhe. Abdallah Ndomondo amesema, kutokana na usemi wa kauli mbiu ya mwaka huu inavyoeleza, Wilaya ya Kibiti inaadhimisha siku hii, kwa kuokota chupa za plastiki katika Kitongoji cha kihingi Pwani hadi bandarini na kutoa elimu ya mazingira kwa Wananchi.
"Kauli Mbiu ya siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka huu imelenga kutafuta suluhisho dhidi ya uchafuzi wa mazingira kwa taka za plastiki". Alisema Ndomondo.
"Lengo la kauli mbiu hii ni kuikumbusha jamii juu ya madhara ya kutumia mifuko ya plastiki na njia bora ya kulejeleza matumizi ya chupa za plastic. Alisema Ndomondo.
Vilevile Mhe. Ndomondo amesema katika ngazi ya Wilaya wamechagua Kijiji cha NYAMISATI kufanyika maadhimisho kwa sababu, kimazingira kuna umuhimu wa kipekee kwani ni lango la maji ya mto Rufiji kuingia baharini ambako kuna Viumbe hai wa aina mbalimbali ambao tunawahitaji kiuchumi na kijamii pia.
" Wananchi wenzangu, tunatakiwa kuyatunza mazingira yetu, ili Viumbe hai wanaopatikana baharini waendelee kuwepo, tuna kila sababu ya kutunza mazingira kwa nguvu zote" Alisema Ndomondo.
Aidha Mhe.Ndomondo amewashukuru wadau wote wa Mazingira na washirika wa Maendeleo kwa kuendeleza ushirikiano na Halmashauri, kutekeleza shughuli za Miradi mbalimbali ya kuhifadhi Mazingira.
"Ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi katika kukabiliana na changamoto za uhifadhi ya mazingira na kuleta maendeleo endelevu nchini" Alisema Ndomondo.
" Ndugu wadau wa mazingira na wananchi kwa ujumla, suala la hifadhi wa mazingira ni letu sote, tunapaswa kulitekeleza kwa vitendo" Alisema Ndomondo.
Akiwa katika shule ya sekondari Wama na kayama, Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira Mhe. Ndomondo ameahidi kuwapelekea miti kumi ya miembe shuleni hapo huku akisisitiza upandaji wa miti ya matunda kwa wingi mashuleni.
Akitoa elimu ya mazingira Afisa Mazingira wa Wilaya ya Kibiti Zakayo Gideon amesema kila mmoja anatakiwa kupinga uharibifu wa mazingira, ikiwa ni pamoja na mifuko ya plastiki.
Hata hivyo Zakayo awewataka wananchi kuiunga SERIKALI mkono katika mapambano dhidi ya mifuko hiyo kwani itupwapo ardhini haiozi, na matokeo yake huzuia au kutengeneza tabaka kati ya udongo wa juu na wa chini na hivyo hata kukiwa na mmea hauwezi kukua, utakufa tuu.
"Kumekuwa na uzalishaji mkubwa wa mifuko ya plastic tena ikiwa feki, na wazalishaji hao wengi hawalipi kodi”. Alisema Zakayo Afisa Mazingira.
Naye Afisa Misitu wa Wilaya Salehe Kilindo amesema mazingira na misitu ni vitu vinavyoshabihiana na kuleta faida mbalimbali hivyo, vyote kwa pamoja vinatakiwa kutunzwa kwa umakini zaidi hususani katika vyanzo vya maji.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamisati Ndg. Hamada Mpangwa amesema, binafsi nifurahishwa sana kwa kijiji cha Nyamisati kuchaguliwa kuwa sehemu ya maadhimisho na kupitia Uongozi wake atahamasisha Wananyamisati kuwa mabalozi wakubwa wa mazingira.
Mwisho baadhi ya wanafunzi wa Sekondari ya Nyamisati na Wama na kayama wamewashukuru wawezeshaji kwa kuwapa mafunzo na kuahidi kuwa elimu hiyo pia nao wataitoa kwa watu wengine hususani katika Jamii wanazotoka.
Katika maadhimisho hayo Afisa MAZINGIRA aliambatana na Afisa Misitu, Afisa Maliasili na Afisa Tarafa wa Kikale.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.