MKUU wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amekutana na Wananchi wa Kijiji cha Nyambili Wilayani humo kwa lengo la kuwatambulisha rasmi mradi mpya wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA chenye thamani ya sh bil.3.5.
"Hii ni bahati wakazi wa Nyambili Kata ya Bungu mmependelewa kwani watoto wenu watapata ujuzi katika chuo hiki,mkilinde" Alisema Kanali Kolombo.
Mradi huo unaotarajiwa kuanza mwezi Juni mwaka huu utakuwa ni msaada mkubwa na mkombozi kwa vijana wa Wilaya ya Kibiti na maeneo mbalimbali kwani chuo kitakuwa na uwezo wa kupokea vijana wengi kwa wakati mmoja.
“Mradi utaanza hivi punde, Sisi ni wasimamizi na watekelezaji wa mradi huu na miradi mingine yote inayotuzunguka “alisema Kanali Kolombo kwa msisitizo huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuitazama kibiti kwa jicho la tatu na kuipatia fedha za ujenzi wa chuo cha Veta.
Kanali Kolombo amesema lengo la Serikali kuanzisha chuo cha Veta ni kuisaidia Vijana ambao hawakubahatika kuendelea na masomo ya Sekondari na chuo, kuweza kupata ujuzi na kuweza kujitegemea wa kufanya shughuli mbalimbali kulingana na fani watakazochagua kujifunza ili kujikwamua kimaisha.
Vilevile Kanali Kolombo amesema ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati kuna kila sababu ya kutoa ushirikiano ili kazi iweze kwenda kwa kasi, kwani kuna baadhi ya miundombinu itapita mashambani kwenu wananchi, kama vile barabara, umeme, maji n.k.
" Ninaomba ridhieni maeneo yenu ambayo mradi utapita, ili tuweze kurahisisha kukamilika kwa mradi ninaomba ushirikiano wenu tusiupoteze huu mradi" Alisema Kanali Kolombo.
Ni matarajio yetu kama ilivyo ada mara baada ya kukamilika kwa ujenzi huu, Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan atakuja kuzindua chuo chetu, hivyo wananyambili jiandaeni kwa ugeni huo mkubwa.
Wakiwa kijijini hapo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji ndg. Denis Kitali amewataka wananchi na Viongozi wa Wilaya kujitoa kusimamia kwa umakini mradi huo, kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa kwa maendeleo ya Kibiti.
Aidha, Mkuu wa chuo cha Ufundi Ikwiriri Bi Ranalda Kyaruzi ambae ndiye Msimamizi wa ujenzi wa chuo hicho, amewataka wananchi wa kibiti kumpa ushirino kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa. Hakuishia hapo pia amewataka wazazi kuwapeleka watoto/vijana wao chuoni ili waweze kupata ujuzi wa fani mbalimbali kwani Veta imesheheni fani kedekede kama vile ujenzi, ushonaji, upishi, umeme wa majumbani n.k
Naye Mratibu wa Elimu Kata ya Bungu Mohamed Mtuliakwako amesema amefurahishwa na taarifa ya mradi na wananyambili wameupokea huku akimpongeza Mbunge wa Jimbo la kibiti Mhe.Twaha Mpembenwe kwa jitihada anazozifanya kuwasemea Wana kibiti hatimaye VETA itajengwa Wilayani Kibiti.
Mwisho wakazi wa Nyambili wakamtoa DC hofu na kumwahidi kuwa, wameupokea na watausimamia mpaka ukamilike. Kuja kwa mradi huu kutasaidia watoto wetu kuacha kuhangaika na masuala ya ajira,tumefurahi Sana .
"Uwezo wa kujitolea tunao, wananyambili ni JADI yetu kujitolea, tunapenda maendeleo chuo kinakwenda kujengwa kwa nguvu zote" Walisema baadhi ya wakazi wa Nyambili Wakiwa na nyuso za furaha wakiwawakilisha wenzao.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.