Hatimaye zao la pamba limerejea Wilaya ya Kibiti kama ilivyokuwa awali ambapo ndilo lilikuwa zao kuu la biashara kabla ya kuimarishwa kwa mazao ya korosho na ufuta. Zao hilo lilipotea kutokana na kulishambuliwa na wadudu na uhaba wa masoko katika miaka ya 1980.
Katika kuhakikisha zao hilo linarejea Jumatatu ya tarehe 12.2.2024 Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amezindua rasmi semina elekezi kwaajili ya kilimo cha pamba Wilayani humo akisema kwamba ni wakati wa Wilaya ya Kibiti kuinuka na kukua kiuchumi.
"Nimefarijika sana kuongezeka kwa zao hili katika Wilaya yangu, sasa kutakuwa na mazao manne ya biashara, kwetu sisi Wanakibiti hii ni neema" Alisema.
Kuongezeka kwa mazao ya biashara kutafanya wakulima kuwa na mzunguko mzuri wa uzalishaji bila kupumzika katika msimu sahihi wa kilimo ukiachilia mbali zao la korosho na ufuta ambayo ni muhimili wa mapato ya Wilaya, hivi karibuni tumeanzisha kilimo cha mbaazi na sasa tunakwenda kuanzisha kilimo cha zao la pamba.
Semina hiyo ililenga kutoa Elimu juu ya Kilimo cha Pamba pamoja na kuwapa ridhaa wawekezaji walioomba kuwezesha kilimo hicho Wilayani Kibiti. Hivyo Kanali Kolombo amewataka wakulima ambao wako tayari kwa kilimo hicho kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiorodhesha majina yao tayari kwa kuanza kilimo cha pamba katika msimu huu bila kuchelewa, kwani mwekezaji amekuja na utaratibu mzuri wa uzalishaji.
"Nimefurahi sana kusikia mwekezaji atawalimia wakulima mashamba yao, atatoa mbegu na kusimamia masoko kwa kuwekeana mikataba na mkulima ambapo mwisho wa siku mkulima atakatwa pesa ile baada ya pamba kuuzwa.
Akimkaribisha Mwekezaji kutoka India Kanali Kolombo amemthibitishia kuwa Kibiti ni eneo salama kwa kilimo, ardhi yake inarutuba ya kutosha, na kazi yake kubwa ni kuhakikisha wananchi wanalima zao hilo sambamba na kupata elimu ya kilimo cha pamba.
Naye Balozi wa Pamba Tanzania ndg, Agrey Mwanri amewataka wakazi wa Kibiti kuhakikisha kilimo cha pamba hakipotei tena Wilayani humo na kupitia zao hilo mapato yataongezeka kwa mkulima mmoja mmoja huku akisisitiza kuwa katika kipindi cha mauzo kila kilo moja itakayouzwa 3% itaingizwa kwenye mfumo wa Halmashauri.
Aidha mwekezaji wa zao la pamba Ndg. Soundar Velusamy ambaye ni kitukuu cha waliokuwa wanunuaji wakubwa wa Pamba ya Rufiji amesema ameamua kuja kuwekeza Kibiti na Rufiji kutokana na historia ya mababu zake, hivyo yuko tayari kushirikiana na wananchi kufufua kilimo cha zao hilo.
"Ukifuatilia historia, pamba ya Rufiji ndiyo pamba yenye ubora zaidi yenye nyuzi ndefu inavyotakiwa kwenye soko la Dunia" Alisema Velusamy.
Naye Diwani wa Maparoni Mhe. Bakari Mpate ambaye ni mbeba maono wa zao la pamba alisema, kipekee amefarijika sana Bodi ya pamba Rufiji kukubali kufufua Tena zao hilo. Zao hilo litaleta tija sana hususani katika mapato ya Halmashauri ya Kibiti.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.