Halmashauri ya wilaya ya Kibiti inafanya juhudi ili kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni ikiwa sehemu ya kumuunga mkono Raisi wa Jamuhuri ya Muungano Tanzania Mhe.Dr Samia Suluhu Hassan ambapo suala la lishe shuleni katika uongozi wa awamu ya 6 limekuwa kipaumbele kuhakikisha watoto wote wanapata chakula shuleni kwa siku zote za shule.
Hayo yamejiri katika kikao cha lishe kwa kipindi cha robo ya pili ambapo idara ya Elimu imetakiwa kuwa na mikakati ya kudumu ya kuhakikisha watoto wanapata chakula wanapokuwa shuleni.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Afisa Utumishi Halima Ngota ameiagiza kamati ya lishe kuhakikisha mambo waliyokubaliana katika kikao hicho yanafanyiwa kazi ili kufikia malengo waliojiwekea.
Akiwakilisha taarifa ya lishe Afisa lishe wilaya ya kibiti Samson Minja amesema wanaendelea na juhudi za kuhakikisha lishe inapatikana katika shule zote ndani ya wilaya ya Kibiti na kuanzishwa kwa bustani. Vilevile amesisitiza uanzishwaji wa club za lishe kwenye shule ambapo mpaka sasa idara ya Lishe imeanzisha shamba darasa la karanga katika Hospitali ya wilaya lengo likiwa ni kutoa hamasa kwenye jamii kuona umuhimu wa uwepo wa Lishe.
Katika kikao hicho idara mbalimbali zimewasilisha taarifa ya hali ya lishe ambapo Afisa Taaluma Mariam msofe wa elimu ya msingi amesema,mpaka sasa shule 48 kati ya 83 zinatoa chakula shuleni wanatarajia kufikia Februari 2023 kuweza kutoa huduma hiyo kwa shule zote huku akisema uhamasishaji unaendelea sambamba na kuwasihi wazazi kuchangia na shule zimeshaanza shughuli za kilimo cha matunda na mbogamboga kwa ajili ya kuboreshwa lishe.
Kwa upande wa elimu sekondari Afisa Elimu Anna Shitindi amebainisha kuwa mkakati wa idara yake mwaka huu ni kuhakikisha shule zote 15 za Sekondari zilizopo zinapata chakula. Licha ya kupatikana kwa chakula ameitaka idara ya lishe na kilimo kupita shuleni kutoa elimu jambo ambalo litakuwa ni chachu ya kuona umuhimu uwepo wa chakula shuleni.
Vilevile idara ya kilimo na mifugo Kaimu Afisa kilimo shemwelwa Bandio na Afisa mifugo Suzan Kawiza wamesema suala la kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji limetekelezwa kwa kutoa ushauri, elimu ikiiwa ni pamoja na kuwasisitiza kuhifadhi vyakula na kuweka akiba ya mifugo kwa matumizi ya baadae, kulima mazao yanayostahimili ukame huku akiahidi kuendelea kushirikiana na idara ya elimu sekondari na msingi kuendelea kutoa elimu ya lishe shuleni.
Aidha Afisa Maendeleo ya Jamii Hamis Mnubi amesema idara yake imefanikiwa kutekeleza upatikanaji wa lishe kwenye Jamii kwa kutoa mikopo kwenye vikundi vya wanawake ,vijana na watu wenye ulemavu .Alifafanua kuwa lengo la mkopo ni kuwawezesha kujiingizia kipato kupitia biashara ndogondogo na kuweza kurahisisha upatikanaji wa chakula na kuboresha chakula kwenye Jamii ambapo fedha hizo pia hutegemea mzunguko kwa namna wanavyorejesha.
Mwisho Mganga Mkuu wa wilaya Daktari Elizabeth Oming'o ameipongeza idara ya elimu kuona umuhimu wa Maafisa lishe na kilimo kufika na kutoa elimu ya lishe shuleni sambamba na kuanzishwa kwa bustani za mbogamboga n.k. Pia amesisitiza kuhakikisha shule zote watoto wanapewa chakula muda wa shule ili waweze kusoma bila ya kuwa na mawazo ya njaa darasani kwani lishe ni kipaumbele kwenye elimu kama Mhe.Rais alivyoelekeza. Pia ameitaka idara ya mifugo kuhamasisha wafugaji kuhakikisha watoto wanapata japo yai moja kwa mwezi Kwa ajili ya kujenga afya zao.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.