Mwenyekiti wa Kamati ya tathmini ya mkataba wa lishe ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ameongoza kikao na kupokea taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa Mkataba ya lishe Wilaya ya Kibiti kwa ngazi ya Kata kwa robo ya nne (Aprili- Juni) ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Akiwasilisha taarifa hiyo kwenye kikao hicho kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Julai 29, 2024 Afisa lishe Wilaya Bi. Roina Daza amesema kamati imefanikiwa kutekeleza shughuli nyingi kwa robo ya nne ikiwemo kuandaa mradi wa lishe kwaajili ya shughuli za mwenge wa uhuru, kufanya vikao vya WDC, kutekeleza kampeni ya ugawaji wa matone ya vitamini A kwa watoto, kutoa Elimu ya lishe, kupima pamoja na kutoa matibabu kwa watoto waliobainika kuwa na utapiamlo mkali.
Aidha Katibu tawala Wilaya ya Kibiti Bi. Maria Katemana ameipongeza kamati kwa jitihada kubwa za utekelezaji wa mkataba huo ikiwemo uwekaji wa taarifa za lishe kwenye mbao za matangazo za vijiji kwa 100% jambo ambalo halikuwa likifanyika hapo awali huku akisisitiza kushirikiana na idara ya kilimo kuhamasisha wakulima kupanda mbegu lishe kama vile mchicha lishe, maharage lishe, viazi lishe n.k.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Ndg. Hemed Magaro amesema tayari amewapatia maelekezo idara ya Kilimo, mifugo na uvuvi kwenye kikao cha lishe cha wataalamu kuhakikisha kuwa wanatoa msaada wa kitaalamu na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara hususani kwenye ngazi ya shule.
“Tumewaagiza wenzetu wa kilimo wahakikishe wanatoa msaada wa kitaalamu, ushauri na kusimamia wakulima kule vijijini bila kusahau shule zetu ili kila shule iwe na bustani za mbogamboga lakini pia kupeleka miche ya mikorosho kwenye shule zenye mashamba makubwa kama Kibiti Sekondari ili mashamba hayo yalete tija” Alisema Magaro.
Akifunga kikao hicho Kanali Kolombo amekitaka kitengo cha lishe kuendelea kuwapatia huduma watoto 71 waliobainika kuwa na udumavu, kufanyia kazi ushauri wa wajumbe wa kuanzisha utaratibu wa kupima hali za lishe za watumishi wa Kibiti ikibidi kuwa na wiki ya lishe Wilaya ili kutoa huduma hizo pamoja na kuwapa elimu wananchi juu ya uongezwaji wa virutubishi kwenye vyakula vyao kama vile unga, mafuta n.k.
Pia Kanali Kolombo amewataka watendaji kutodharau jitihada zao kwani malengo ya kata yakifikiwa ndivyo Halmashauri, Mkoa na Taifa litakavyofikia malengo yake.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.