Idara ya Elimu divisheni ya elimu ya Awali na Msingi Wilaya ya Kibiti imefanya kikao kazi chenye lengo la kujitathmini kiutendaji na kutafuta mapinduzi ya elimu kutokana na changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na matokeo ya darasa la 4 na la 7 kuwa mabaya.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Elimu Awali na Msingi,katika kikao hicho kilichofanyika shule ya msingi kitundu Afisa Elimu Taaluma Msingi Hamis Athman Shemahonge amesema hali ya matokeo hairidhidhi Kwa ujumla kuna kila sababu ya kila Mwalimu kujitathmini mwenyewe kuwa anafanya nini.
Akisoma Hali halisi ya matokeo Shemahonge amesema jumla ya Wanafunzi 5633 walisajiliwa kufanya mtihani wa darasa la Saba Waliofanya mtihani ni 5597 na Kati Yao 4058 wamefaulu mtihani huo sawa na asilimia 72.5 za ufaulu.
Kwa upande wa mtihani wa upimaji wa darasa la nne jumla ya Wanafunzi 5826 waliosajiliwa 5622 walifanya mtihani na kati Yao 4615 walifaulu mtihani huo .
Kwa nyakati tofauti Walimu katika muda wa majadiliano ya kubaini chanzo cha matokeo mbaya wamesema hali ya ufaulu duni wa wanafunzi katika wilaya umewahuzunisha sana hata wao hawafurahishwi na kitendo hicho.
“Wazazi wanatuhujumu watoto kufanya vibaya mitihani Wilaya ya Kibiti hatufurahishwi tunaumia sana”walisema Walimu.
Katika mjadala huo Walimu wamebainisha baadhi ya changamoto zinazochangia ufaulu duni kubwa likiwa ni Ushawishi wa jamii hasa kwa wazazi kuwaambia wanafunzi wafanye vibaya kwenye mitihani yao na mfano ni kilichotokea Kitembo,Nyamatanga na Machipi kama matokeo yanavyoonyesha.
Vilevile wamesema Kukosekana msimamo wa pamoja kama wilaya katika uendeshaji wa kambi za kimasomo kwa ajili ya maandalizi pia huchangia watoto kushindwa kufanya vizuri katika mitihani yao.
Wakiendelea kutoa masikitiko yao Walimu wakati wa mjadala huo wamesema Utendaji duni kwa baadhi ya walimu katika suala zima la ufundishaji ,Usimamizi pamoja ufuatiliaji hafifu unaofanywa na viongozi wa kielimu katika ngazi zote yaani Shule,Kata na Wilaya pia huchangia upatikanaji wa matokeo mabaya Kwa sababu ya kushindwa kutekeleza majukumu yao Kwa wakati .
Hata hivyo Walimu wamelalamikia suala la kukosekana kwa motisha linawarudisha nyuma na linawakatisha tamaa sana kwani hakuna kazi isiyokuwa na motisha huku wakilalama Kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa serikali za mitaa pindi wanapohitaji msaada kutoka ngazi hiyo.
Mara baada ya majadiliano kikao hicho kilichoshirikisha Idara ya Elimu ngazi ya wilaya,Kata na shule Kwa pamoja wameazimia Viongozi wa ngazi ya wilaya kupita katika Kata na Vijiji kuwaelimisha wazazi kuhusu haki ya wanafunzi kusoma na kuwaacha wafaulu mitihani yao ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua Kwa vitendo wazazi wenye tabia hizo, ikiwa ni pamoja na kulipa faini na kufikishwa mahakamani.
Vilevile wameazimia Viongozi wote kuwa na nguvu za kiutawala katika kusimamia ufundishaji shuleni kwa kufuata kanuni na taratibu na maelekezo ya kazi,na kuanzia sasa Mwalimu mkuu ambaye anaona hataweza kupendana na kasi tunayoanza ni vyema akajitoa mapema kupisha atakayeweza kufanya kazi.
Katika hatua nyingine wameazimia Maafisa Elimu Kata wote kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara katika shule zao na kutoa taarifa kwa Afisa Elimu Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji juu ya kinachojiri katika ngazi ya shule
Aidha wamesema walimu wakuu wakahakikishe kuwa suala la nidhamu kwa wanafunzi na walimu linasimamiwa kikamilifu kuhakikisha maadili yanakuwepo katika Taasisi hiyo.Pia wameazimia Kuimarisha mahusiano mazuri na viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa katika kusimamia mahudhurio ya wanafunzi shuleni
Awali Katibu wa chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Kibiti Mwalimu Crecencia Tingwa aliipongeza idara Kwa kuitisha kikao hicho mapema kwani kitatoa mtazamo wa nini kifanyike kuleta mapinduzi ya Elimu kibiti . Vilevile Mwalimu Tingwa amesema ili kupata utendaji chanya Walimu lazima washirikiane na kufanya kazi kwa upendo huku aliwasisitiza Walimu wote ambao hawajajiunga na chama cha Walimu kujiunga kwani ni chama imara cheye kuwasemea changamoto zao na kupata muafaka kwa wakati.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.