8.12.2023.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo ameongoza watumishi kushiriki kufanya shughuli za kijamii katika soko la Kibiti ikiwa ni siku moja kabla ya kuadhimisha sikukuu ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Kanali Kolombo amewashukuru watumishi na wananchi wote waliojitokeza kufanya usafi wa mazingira katika eneo la soko hilo ambapo shughuli zilizofanyika ni kufyeka nyasi, kufagia na kukusanya takataka.
"Suala la usafi lilianza siku nyingi, wakati Taifa likiwa na miaka 12, ilipishwa kampeni ya usafi ( Mtu ni Afya) ambayo iliasisiwa na Baba wa Taifa Mwl J.K . Nyerere." Alisema Kolombo.
Vilevile Kanali Kolombo aliwaalika watu wote kujitokeza kushiriki mdahalo ambao ulijadili mafanikio mbalimbali kabla na baada ya uhuru, huku akialika wazee wa zamani waliopo Kibiti ambao waliweza kutupatia shuhuda namna mambo yalivyokuwa kabla ya uhuru na muelekeo wa wilaya yetu baada ya uhuru.
"Siku ya kesho ni kilele cha maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru Tanzania, tumealika wazee wetu na hivyo mjitokeze kwa wingi kusikiliza mdahalo huo" Alisema Kolombo.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Wilaya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Bw. Hemed Magaro alisema zoezi hilo la usafi ni maagizo maalumu kutoka Mkoani kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais
"Tulipofika hapa eneo hili lilikuwa pori lenye nyasi ndefu, lakini baada ya kujitoa kwetu tumeweka mazingira haya kuwa safi, hongereni sana" Alisema Bw. Magaro.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa Disemba 3 katika kilele cha Tamasha la Bibititi Mohammed wilayani Rufiji ikiwa ni maelekezo ya Mhe. Rais.
"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. SSH ameagiza maadhimisho yafanyike kimkoa na kiwilaya kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, mijadala sambamba na kuzindua mchakato wa dira ya maendeleo ya Taifa 2025-2050" Alisema Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa.
Tukio hilo la usafi wilayani Kibiti limehusisha watumishi wote wa Halmashauri ya Kibiti, Taasisi mbalimbali likiwemo jeshi la Polisi, jeshi la Magereza, TAKUKURU, Benki ya NMB, TANESCO, TARURA pamoja na Wananchi wa Kibiti.
Pichan ni matukio mbalimbali ya zoezi hilo la usafi katika soko la Kibiti.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.