Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na Tanzania kwa ujumla imeungana na nchi nyingine ulimwenguni kuazimisha siku ya uvuvi Duniani yenye kauli mbiu ya Bahari ni kioo chetu , katika kijiji cha Pombwe kata ya Ruma Tarafa ya Mbwera wilayani humo.
Maadhimisho hayo huadhimishwa Kila mwaka ifikapo Novemba 21 kwa lengo la kuwakumbusha wavuvi, namna sahihi ya kuzingatia taratibu na Sheria za uvuvi hususani katika zana za kuvulia, kuchukua tahadhali wanapokua katika kazi za uvuvi baharini pia kutengeneza umoja wa wavuvi ili kwa Pamoja waweze kutatua changamoto zinazowakabili na kuelekezana njia sahihi za uvuvi.
Hayo yamebainishwa na Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Kibiti Japhet Manyama alipokuwa akitoa ufafanuzi wa maadhimisho hayo wakati akimkaribisha mgeni rasmi kwenye hafla hiyo kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha pombwe.
Akizungumza AfisaTarafa ya Mbwera Lucas Magai kwa niaba ya mkuu wa Wilaya ya Kibiti Meja Edward Gowele ambaye alikua mgeni rasmi katika hafla hiyo, amewapongeza wakazi wa Kijiji hicho kwa namna walivyojitokeza katika maadhimisho hayo na amewasisitiza wakazi hao kushirikiana na BMU kuhakikisha hali ya usalama inakua shwari katika Kijiji cha pombwe huku akiwataka wakazi hao kutoa taarifa za wageni wanaoingia na kutoka katika kisiwa hicho. Pia Magai amependekeza kuanzishwa kwa mafunzo ya mgambo kwa vijana wanaotoka katika jamii inayoishi delta ili kuimarisha hali ya usalama kwa muda wote visiwani .
Vilevile Magai amewataka wakazi hao kuchukua tahadhari juu ya magonjwa mbalimbali kama vile UKIMWI na CORONA kutokana na mwingiliano wa watu, kwani hivi karibuni nchini china kumetokea vifo vya watu takribani 6 waliopoteza maisha kwa ugonjwa wa corona jambo ambalo wengi huamini kuwa ugonjwa huo umekwisha kutoweka.
Afisa Tarafa Magai amekemea suala la utoro mashuleni katika maeneo ya uvuvi na kuwataka wazazi kutekeleza majukumu yao kwa kusimamia na kuhakikisha watoto wanakwenda shule sambamba kuwapa mahitaji, Pia amesema kuwa Serikali imesimamia elimu bila malipo darasa la kwanza mpaka kidato cha 6 Ili kuhakikisha Kila mtoto anapata elimu.
Pamoja na hayo Bw. Magai amewaagiza wakazi wote wa delta ikiwa ni pamoja na kina Mama kuunda vikundi vitakavyowasaidia kupata mikopo ya kufanyia biashara mbalimbali ili kuweza kjikwamua kimaisha na kuwasihi wavuvi kuwekeza fedha wanazozipata kwa manufaa ya baadae.
Aidha sherehe hiyo ilitumbuizwa kwa michezo mbalimbali kama vile kuvuta kamba kukimbia, kuogelea, kuvusha mitumbwi, maigizo na mashairi yaliyosheheni vina vyenye maudhui ya matumizi sahihi ya Bahari na rasilimali zake sambamba na zoezi la kutoa zawadi kwa Washiriki wa michezo hiyo.
Mwisho Magai ameahidi kuzibeba changamoto zilizopo kijijiji hapo kwa kuzifikisha katika ngazi husika hususani kupata muafaka wa uhakika wa mmiliki halali wa kisiwa cha Simaya kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na kilwa.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.