Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo amewataka wazazi , walimu na bodi ya shule kusimamia maadili ya watoto katika mazingira wanayoishi kuhakikisha wanawajengea nidhamu itakayowawezesha kuishi na jamii vema wakiwa shuleni na baada ya kumaliza shule.
“malezi ya watoto ni jukumu letu sote,tushirikiane kufuatilia maadili ya watoto hasa huko mabwenini wanakolala na wanapokuwa majumbani” alisema Kolombo.
Amesema hayo katika mahafali ya 23 ya shule ya Sekondari ya wavulana kibiti ambapo alikuwa ndiye Mgeni rasmi pia ametoa pongezi kwa Mhe. Rais Dr.Samia Suluhu kwa kuwekeza fedha nyingi katika idara ya elimu. Sambamba na hilo amepongeza jitihada zote na Walimu,wazazi na walezi kuhakikisha ufaulu unaongezeka shuleni bila kujali changamoto zinazojitokeza kwa kujitoa kuunga mkono jitihada zinazofanywa shuleni hapo kwa hali na mali.
“Jitihada zenu zimeleta ufaulu mzuri, endeleeni na utaratibu huu tuweze kutokomeza zero kibiti” alisema Kanali Kolombo.
Akijibu changamoto zilizoainishwa katika risala ya Mkuu wa shule ,wanafunzi wanaomaliza na wanaobaki Kanali Kolombo amesema amezibeba na ameahidi kuzifanyia kazi kwa kushirisha na Halmashauri au taasisi nyingine ili kuweza kutatua changamoto hizo.
Aidha akiwa shuleni hapo Kanali Kolombo ameahidi kuchangia sh 500,000 kwa ajili ya kuendeleza mradi wa kutengeza sabuni unaofanywa na klabu ya wanafunzi wajasiliamali shuleni hapo, pia ameahidi kuchangia kiasi cha shilingi 300,000 kwa ajili ya kuunga Mkono jitihada za wazazi katika kuunga Mkono shughuli za Kitaaluma shuleni hapo.
Kwa nyakati tofauti wakisoma risala ya wanafunzi pamoja na taarifa ya Mkuu wa shule wamesema, shule imekuwa na mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupandisha ufalu wa wanafunzi kwa miaka sita mfululizo licha ya kuwa bado wanakabiliwa na changamoto kadha wa kadha kama vile uvamizi wa eneo la shule, kukosa mfumo wa kisasa wa gesi ya kupikia chakula cha wanafunzi, upungufu wa samani na ukosefu wa usafiri wa shule kwa muda mrefu, upungufu wa vitabu vya kiada na ziada, na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na Hesabu.
Katika hatua nyingine Katibu wa jumuiya ya wazazi shuleni hapo Mhandisi Kaiza John ameendesha Harambe na kupata zaidi ya sh. milioni moja lengo likiwa ni kusaidia kukwamua changamoto za shule ikiwa ni pamoja na kulipa mshahara wa walimu watatu wanajitolea kufundisha shuleni hapo kutokana na upungufubwa walimu pia wanatarajia kununua mashine ya kudurufu (photocopy mashine).
Naye Meneja mahusiano wa huduma za wateja wa Azania Bank ndg. Othman Jebra (mwanamfunzi wa Kibiti sekondari miaka ya nyuma ) akiwa ameambatana na Afisa mahusiano wa Bank hiyo Bakari Mmbaga wametoa zawadi kwa washindi wa 3 waliofanya vizuri zaidi katika mitihani yao, ambapo mshindi wa kwanza amepata sh150,000, mshindi wa pili amepata sh 100,000 na mshindi wa tatu amepata sh 70,000. Jebra amesema wametoa zawadi ili kutoa hamasa kwa wanafunzi kusoma kwa bidii na kurudisha shukrani kwenye jamii hususaani katika shule aliyosoma miaka kadhaa iliyopita huku akiwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri mitihani yao ya kumaliza kidato cha 6.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.