Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), imeendelea kutoa elimu kwa Umma katika shule za Sekondari zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Kibiti katika mkoa wa Pwani. Lengo likiwa ni kuongeza uelewa kwa jamii hususani kwa wanafunzi ili wawe mabalozi wazuri kwa jamii inayowazunguka.
Mkaguzi wa Dawa kutoka TMDA Kanda ya Mashariki Bi. Joy Hezekieh amesema, elimu hiyo kwa wanafunzi ni pamoja matumizi sahihi ya dawa pamoja na madhara yatokanayo na matumizi yasiyo sahihi ya dawa, mfano cheti cha dawa kimeandikwa 2x3(2 inawakilisha idadi ya vidonge ambavyo mgonjwa anatakiwa kutumia kwa wakati huo na 3 inawakilisha masaa, siku 1 ina masaa 24 ukigawanya kwa 3 unapata masaa 8, hivyo mgonjwa atatakiwa kutumia vidonge vyake kila baada ya saa 8). Neno kutwa huleta maana isiyo sahihi kimantiki, huwafanya wagonjwa wameze dozi nzima ya dawa kwa mgawanyiko wa saa 12 pekee.
Akizungumzia njia sahihi ya uteketezaji wa dawa zilizokwisha muda wa matumizi, Bi Joy awamewataka kutokutupa hovyo dawa zilizokwisha muda wa matumizi majumbani badala yake wapeleke kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vilivyo karibu.
Pia wamewaelekeza jinsi ya kuripoti madhara ya dawa(adverse drug reaction) kwa kupiga namba ya bure 0800110084 pamoja na *152*00# kisha unachagua afya baadaye TMDA na kufuata maelekezo,
Aidha TMDA imewataka wanafunzi hao kuacha tabia za kutumia dawa pasipo kupima, wametakiwa kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pindi wanapohisi dalili za ugonjwa ili waweze kupata matibabu sahihi na kwa ugonjwa sahihi. Mbali na hayo TMDA imeitaka jamii kuacha mtindo wa kutumia maduka ya dawa muhimu kama sehemu yakupata huduma za maabala na kitabibu.
Mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) ni Taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya yenye jukumu la kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, Usalama na Ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.