Ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Mwenyekiti wa Siasa Itikadi na Uenezi Mkoa wa Pwani Mhe. Mwinshehe Mlao ameendelea kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Mkoa wa Pwani ambapo Jana tarehe 21.02.2024 ilikuwa ni zamu ya Wilaya ya Kibiti.
"Lengo la ziara yangu ni kusikiliza na kutatua kero na changamoto za wananchi, ndiyo maana mnaona nimebatana na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wataalam wa Halmashauri" Alisema Mhe. Mlao.
Mara baada ya kusikiliza kero za wananchi waliojitokeza Mhe. Mlao amewaagiza Wakuu wa Idara wote (wataalam), kuyafanyia kazi yote waliyoelezwa na kuyabeba kisha kupeleka mrejesho kwenye Chama ngazi ya Wilaya na Mkoa kupitia maswali ambayo haya kupatiwa majibu katika mkutano huo.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo alijibu maswali ya changamoto na kero zilizojitokeza katika mkutano huo, pia alipokea kero ambazo hazikupata majibu ya papo kwa papo na kuahidi kuzifanyia kazi kwa kadri itakavyowezeka ili kuhakikisha wananchi wa Kibiti wanaishi wakiwa na amani na furaha kwa rasilimali walizonazo.
Katika ziara hiyo Mbunge wa Jimbo la Kibiti Mhe. Twaha Mpembenwe amemshukuru Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mhe. Mwinshehe Mlao kwa kuona haja ya kuitembelea Kibiti sambamba na pongezi nyingi kwa Mhe. Rais Dkt. SSH kwa kuiletea Kibiti fedha nyingi kwaajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Zaidi ya yote Mhe. Mpembenwe amewasihi wananchi na wanachama wa vyama vyote Kibiti kuendelea kumwamini na kuwa na mshikamano wakati akiendelea kuchapa kazi kwa nguvu zote lengo kuu likiwa ni kuhakikisha Kibiti inasonga mbele.
"Naomba mniamini, mna Mbunge makini, ninaendelea na nitaendelea kushirikiana na nanyi mpaka nihakikishe maendeleo ya Kibiti yanaimarika, kikubwa tuimarishe upendo hivyo nawaahidi tutafika salama" Alisema Mhe. Mpembenwe.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge amesema kwa Wilaya ya Kibiti mwaka 2024/25 ni mwaka wa ujenzi na kilimo ambapo hivi sasa ajenda kuu ni kuhakikisha Wilaya ya Kibiti inakuwa na viwanda vya kutosha na kupandisha mapato ya Wilaya.
"Tutumie vizuri fursa hii kuhakikisha Kibiti inakuwa na viwanda, tayari nimemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji kutafuta maeneo ili tuweze kuleta wawekezaji na inawezekana" Alisema Kunenge.
Wakizungumza na hadhara iliyojitokeza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa Mhe Johnson na Mwenyekiti wa UWT Mkoa Mhe. Zainabu Vullu wao wamesema ili kuweza kufikia malengo uwepo wa viongozi bora unahitajika ndani ya Chama na siyo kuwa na bora viongozi, hivyo wamewasisitiza wanachama hao kuwa na nidhamu, umoja, amani na kuufanya upendo kuwa nguzo ya utendaji baina yao na si vinginevyo.
Awali akifungua Mkutano huo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibiti Mhe. Juma Ndaruke alisisitiza kuwa, mahusiano ya Chama na Serikali ni imara, huku akiwapongeza Waheshimiwa Madiwani, Mhe. Mbunge na Viongozi wote wa Chama kwa namna wanavyopambana kuhakikisha Kibiti inapata maendeleo.
Kero zilizotolewa na wananchi kutoka Kata, vijiji na Vitongoji mbalimbali kwa asilimia kubwa zilikuwa na mfanano kama vile uhitaji Barabara, fidia, vituo vya Afya, zahanati, malalamiko ya mgambo kukamata wajasiriamali wanawake, tozo kwa wauza mbogamboga, tozo za mazao n.k.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.