WAZEE WATHIBITISHA UWEPO WA MAENDELEO NDANI YA MIAKA 62 YA UHURU.
9.12.2023.
Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti imeungana na Wilaya nyingine zote nchini kusheherekea maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania bara.
Sherehe hizo zimefanyika kwenye kila Wilaya nchini ikiwa ni maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. SSH aliyeagiza sherehe hizo kufanyika kwa kufanya shughuli za kijamii, mijadala na uandaaji wa dira ya Taifa 2025 - 2050.
Kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, shughuli za kijamii zilizofanyika ni: kufanya usafi katika eneo la soko la Kibiti kisha kufuatiwa na mchezo wa kirafiki wa mpira wa miguu kati ya timu ya KURUGENZI FC na KIBITI UNITED uliofanyika katika Uwanja wa Samora – Kibiti, ambapo timu hizo zilitoka sare ya goli 1-1, mambo haya yalifanyika siku moja kabla ya maadhimisho yaani tarehe 08-12-2023.
Pia kulifanyika Mashindano ya insha na utunzi wa ushairi mashuleni wiki moja kabla ya sherehe hizo na washindi wote walikabidhiwa zawadi tarehe 09-12-2023, siku ya maadhimisho hayo ambayo yalifanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri. Sambamba na hilo siku hiyo pia ulifanyika mdahalo uliowashirikisha WAZEE MAARUFU ambao waliweza kuelezea kinagaubaga maendeleo yaliyofikiwa ndani ya Wilaya kwa kipindi cha miaka 62 ya UHURU.
Akichokoza mada kabla ya mdahalo kuanza, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bw. Hemed Magaro alichagiza kwa kuelezea maendeleo yaliyopatikana katika miaka 62 ya UHURU ndani ya Wilaya hivyo kuonesha namna ambavyo Kibiti imepiga hatua kubwa kimaendeleo.
Magaro amesema Licha ya Halmashauri kuwa changa mpaka sasa kuna ongezeko kubwa la shule za Msingi na Sekondari,vituo vya Afya, zahanati ongezeko la chakula katika Sekta ya Kilimo na pato la Wilaya limeongezeka .
Aliendelea kusema kuwa pato la Wilaya limeongezeka kutoka makusanyo ya 9,390,000 mpaka kufikia Bil 1.18 na tunatarajia kukusanya takribani bil 2 na point kadhaa kwa mwaka huu, haya ni maendeleo makubwa.
Vilevile Mhandisi Ayubu Ngereza amesema kwa upande Barabara ,maji na umeme Wilaya imepiga hatua kubwa ambapo mpaka sasa Barabara nyingi zinapitika na maeneo mengi kufikika, mpaka sasa 68.4% ya wakazi wa Vijijini na 67% ya wakazi wa mjini wanapata maji kutoka vyanzo mbalimbali vya maji ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Aidha wazee wa zamani wa Kibiti walioshiriki mdahalo kwa nyakati tofauti, wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana nchini kwani kila mwenye macho anaona haambiwi tazama.
Katika awamu zote za uongozi tumepiga hatua, Sasa tuna shule nyingi, vituo vya Afya, zahanati, Barabara zinaendelea kujengwa na zinapitika, huduma za maji na umeme zinapatikana pamoja na kwamba bado kuna changamoto .
Wazee hao kwa umoja wao wamewataka viongozi wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia vizuri kila kitu kilichopo ili kuleta maendeleo zaidi, huku wakiwataka kufufua mambo mengine ambayo hayakuwezekana katika kipindi cha miaka ya nyuma, kama vile kilimo cha zao la pamba ambalo ndilo lilikuwa zao la biashara Wilayani Kibiti kabla ya kushamiri kwa mazao ya korosho na ufuta.
"Katika maadhimisho haya tulipewa maelekezo na Mhe. Rais tumetekeleza kwa kufanya yote tuliyoagizwa ikiwa ni pamoja na kuandaa mdahalo huu kujadili mafanikio yaliyofikiwa katika wilaya yetu" Alisema Kolombo.
"Kama mlivyosikia katika mdahalo, wazee wamekiri kuwepo kwa maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali za mahitaji muhimu ya kila siku ikiwemo miundombinu yote kama vile Elimu, Afya , Maji, Barababa, Umeme, Kilimo, Ongezeko la pato la wilaya n.k.
Kanali Kolombo amesema Serikali inaendelea kufanya jitihada kubwa kuhakikisha maendeleo yanapatikana ndiyo maana inaendelea kuleta fedha mbalimbali za kutekeleza miradi katika wilaya yetu.
"Nimesikiliza mdahalo kwa makini wazee wangu nimewasikia mawazo, maoni , ushauri nimeyabeba na Serikali yetu ni sikivu, ninaimani yote mliyowasilisha leo yatatekelezwa" Alisema Kolombo.
Vilevile Kanali Kolombo kupitia kauli mbiu ya maadhimisho hayo ya Uhuru mwaka 2023 isemayo MIAKA 62 YA UHURU, "UMOJA NA MSHIKAMANO NI CHACHU YA MAENDELEO YA TAIFA LETU" amewataka Wana kibiti kuhakikisha wanakuwa na UMOJA na MSHIKAMANO kuhakikisha Kibiti inasonga mbele.
Akihitimisha maadhimisho hayo, Kanali Kolombo amewataka wazazi na walezi katika kipindi hiki cha likizo kuhakikisha wanawaandikisha shule watoto wote wenye umri wa kuanza darasa la Awali na Msingi katika shule mbalimbali zilizopo hapa Wilayani kwani kupata Elimu ni haki ya kila Mtanzania.
"Ndugu zangu ni wakati wa likizo hakikisheni watoto wenye umri kati ya miaka 4-6 wanaandikishwa madarasa ya Awali na Msingi na wale darasa la saba waliofaulu wanapelekwa shule za sekondari kama watakavyopangiwa, kwa yeyote ambaye hatofanya hivyo hatua za kisheria ziitachukuliwa" alisema Kolombo.
Copyright ©DED-KIBITI 2017 . All rights reserved.